Lugha Nyingine
Kampuni za kigeni zaendelea kuwa na imani katika ukuaji wa China kutokana na Mpango wa 15 wa Miaka Mitano

Picha ikionyesha treni za mizigo zinazotoa huduma kati ya China na Ulaya zikisubiri kuondoka katika Stesheni ya Reli ya Manzhouli, inayoendeshwa na Kundi la Shirika la Reli la China Tawi la Harbin mjini Manzhouli, Mkoa wa Mongolia ya Ndani, Kaskazini mwa China, Februari 26, 2026. (Picha na Huang Xu/Xinhua)
Wakati wa kipindi cha Mpango wa 14 wa Miaka Mitano (2021-2025), Pato la Taifa la China lilivuka vikomo mfululizo, likizidi yuan trilioni 110 (Dola za Marekani karibu trilioni 15.8), yuan trilioni 120, yuan trilioni 130 na halafu yuan trilioni 140, likiwa na wastani wa kiwango cha ukuaji wa kila mwaka wa asilimia 5.4, juu zaidi kuliko wastani wa kiwango hicho duniani.
Mpango wa 15 wa Miaka Mitano (2026-2030) kwa mara nyingine tena unaipa dunia maono yaliyo wazi, tulivu na yanayotabirika ya maendeleo. Huku uchumi wa China ukiwa katika msingi imara zaidi, ukisonga mbele na mwelekeo dhahiri zaidi wa ukuaji na kuonyesha uhimilivu zaidi, idadi inayoongezeka ya kampuni za kigeni zimefikia hitimisho moja: kukita mizizi China na kutafuta maendeleo ya pamoja.
Lin Chunmei, makamu mkuu wa Corning Incorporated ambaye pia ni mkuu na meneja mkuu wa Corning Greater China, ameiambia People's Daily Online kwamba Mpango wa 15 wa Miaka Mitano wa China unajikita katika kuhimiza maendeleo yenye sifa bora kwa kukuza nguvu mpya za uzalishaji zenye sifa bora na kufikia kiwango cha juu zaidi cha kujitegemea na nguvu kubwa zaidi katika sayansi na teknolojia.
“Mpango huo pia unaweka malengo dhahiri ya kupanua ufunguaji mlango wa kiwango cha juu, kuhimiza ufunguaji mlango wa taasisi na kuendana na sheria za kimataifa,” Lin amesema. Ameeleza kuwa hiyo si tu inapanga njia kwa ukuaji wa uchumi wa China lakini pia inatengeneza fursa mpya kwa kampuni za kimataifa kukua pamoja na viwanda vya China.
"DHL Express kwa muda mrefu imekuwa ikiwa na maono mazuri juu ya soko la China, na dhamira yetu ya kuwekeza hapa bado ni imara," amesema Wu Dongming, Mkurugenzi Mtendaji wa tawi la China la DHL Express, kampuni ya Ujerumani inayotoa huduma ya uchukuzi, katika mahojiano na People's Daily Online.
Mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 40 tangu kuanza kwa shughuli za DHL Express nchini China. Katika kipindi hicho cha miongo zaidi ya minne, kampuni hiyo imeshuhudia na kuchangia kikamilifu katika kuibuka na kujumuishwa kwa uchumi wa China katika uchumi wa dunia, Wu amebainisha.
"Tukiangalia kipindi kijacho cha Mpango wa 15 wa Miaka Mitano, tutaendelea kuongeza kwa kina uwekezaji wetu, kuimarisha uwezo wetu wa huduma na kutoa uungaji mkono imara kwa kampuni za China zinazokwenda kimataifa," Wu amesema.
Anna An, mkuu wa Henkel Greater China, amesema soko la China limeonyesha uhimilivu mkubwa na uwezo wa ukuaji wa muda mrefu, na kwamba kampuni hiyo ina imani kamili katika maendeleo ya uchumi wa China wakati wa kipindi cha Mpango wa 15 wa Miaka Mitano.
Mwaka wa 2026 ni wa maadhimisho ya miaka 150 tangu kuanzishwa kwa Henkel na mwaka wa 55 tangu kampuni hiyo iingie China. An amesema kampuni hiyo itaendelea kuwekeza katika uvumbuzi, uzalishaji bidhaa na ukuzaji wa vipaji vya China, na kuongeza kwa kina juhudi zake za ujanibishaji kuendana na malengo ya maendeleo yenye sifa bora ya Mpango wa 15 wa Miaka Mitano.
Ni nini chanzo cha imani hii miongoni mwa kampuni za kigeni nchini China?
Liu Yunfeng, makamu mkuu mtendaji wa Kundi la Volkswagen Tawi la China, ameiambia People's Daily Online kwamba soko kubwa la ndani la China linabaki kuwa kivutio kikubwa. “Sifa bora za nchi hiyo katika uwezo wa viwanda, miundombinu na uvumbuzi huunda mchanganyiko ambao ni vigumu kwa nchi zingine kuufikia,” Liu amebainisha, akiongeza kuwa sifa hizo bora zinaunda msingi imara wa maendeleo ya muda mrefu ya uchumi wa China.
Katika dunia yenye mabadiliko na misukosuko, kuongezeka kwa hatua za upande mmoja na kujihami, na hali inayosusua ya kuimarika kwa uchumi duniani, hali ya uhakika imekuwa rasilimali adimu. Kinyume na hali hiyo, China inaendelea kuchangia asilimia karibu 30 ya ukuaji wa uchumi duniani, ikitumika kama nanga ya utulivu inayoaminika.
China inaendelea kujitolea katika kuungana mikono badala ya kurusha ngumi, kuondoa vizuizi badala ya kujenga kuta, na kuhimiza muunganisho badala ya kutengana. Nchi hiyo inaendelea kukumbatia dunia kwa mikono miwili, ikitoa chanzo thabiti na cha kuaminika cha hali ya uhakika. Mpango wa 15 wa Miaka Mitano unapoanza, China iko tayari kufanya kazi na nchi zote kuchangia dunia fursa zake za maendeleo na kuweka dira kuelekea ustawi wa pamoja duniani.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



