Waziri wa Mambo ya Nje wa China ahimiza mazungumzo ya amani katika mazungumo kwa simu na mwenzake wa Iran

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 25, 2026

BEIJING - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi jana Jumanne katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na mwenzake wa Iran Seyed Abbas Araghchi amesema kwamba matatizo yote makubwa yanapaswa kutatuliwa kupitia mazungumzo na majadiliano, badala ya kutumia nguvu.

Araghchi amemwelezea Wang hali ya sasa ya kikanda. Akiishukuru China kwa kutoa msaada wa dharura wa ubinadamu, amesema watu wa Iran wako na mshikamano zaidi katika kupinga uchokozi kutoka nje na kulinda mamlaka ya nchi na uhuru wa nchi hiyo.

"Iran imedhamiria kufikia kukomesha vita kikamilifu, badala ya kusitisha mapigano kwa muda tu," Araghchi amesema, akisisitiza kwamba Mlango Bahari wa Hormuz uko wazi kwa nchi zote, na meli zinaweza kupita salama, lakini nchi zinazopigana na Iran haziko katika hali hii.

Ameeleza matumaini kwamba hatua zinazochukuliwa na pande zote zitasaidia kupunguza hali ya kupamba moto kwa mgogoro, akitarajia China kuendelea kufanya juhudi katika kuhimiza amani na kumaliza vita hivyo.

Kwa upande wake, Wang, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), amesisitiza msimamo wa kikanuni wa China, akisema ni bora kufanya mazungumzo kuliko kuendelea na mapigano.

"Hii inatumikia maslahi ya Iran na watu wake, na pia inaonesha matarajio ya pamoja ya jumuiya ya kimataifa," amesema.

Wang ametoa wito kwa pande zote kwenye mgogoro huo kutumia kila fursa na dirisha za amani, na kuanzisha mazungumzo ya amani mapema iwezekanavyo.

"China itaendelea kushikilia msimamo wa haki unaofuata hali halisi, kupinga kuvamia mamlaka ya nchi nyingine, kufanya juhudi za kuhimiza amani na usimamishaji mapigano, na kufanya juhudi kwa ajili ya amani na utulivu wa kikanda," Wang amesema.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha