Lugha Nyingine
Marekani yatuma mpango wa amani wa masharti 15 kwa Iran kupitia Pakistan
WASHINGTON - Marekani imetuma mpango wa amani wa masharti 15 kwa Iran, kupitia Pakistan, katika jaribio la kumaliza vita na Iran, ambavyo sasa vipo katika wiki yake ya nne, Gazeti la The New York Times limeripoti jana Jumanne, likirejelea maafisa wawili ambao hawakutajwa majina.
Ripoti imesema, utawala wa Trump una shauku ya "kupata njia ya kutoka kwenye mgogoro huo kutokana na kukabiliana na athari zake za kiuchumi."
Ripoti hiyo imesema kwamba mpango huo unashughulikia mipango ya makombora ya balestiki na nyuklia ya Iran na kujadili njia za baharini, ikirejelea Mlango-Bahari wa Hormuz.
Hata hivyo, ripoti hiyo inasema kwamba, haikuwa wazi namna mpango huo mpana, uliowasilishwa kupitia njia ya Pakistan, umeweza kutumwa miongoni mwa maafisa wa Iran na kama Iran itaweza kuukubali kama msingi wa mazungumzo.
"Pia haikuwa wazi kama Israeli ilikuwa ikikubaliana na pendekezo hilo," ripoti hiyo imeongeza.
Chaneli ya 12 ya Israeli pia imeripoti siku hiyo ya Jumanne kwamba Washington imewasilisha kwa Tehran mpango wa masharti 15 kwa ajili ya makubaliano ya kusimamisha mapigano kwa mwezi mmoja.
Chaneli hiyo ya TV, ikirejelea vyanzo vinavyofahamu jambo hilo, imesema washauri wa Rais Donald Trump wa Marekani, Steve Witkoff na Jared Kushner, wanahimiza mpango huo kwa kusimamisha mara moja uhasama, kwa kutumia kipindi cha siku 30 kukamilisha mpango huo wa masharti 15.
Mpango huo unataka kwamba Iran ivunje uwezo wake wa nyuklia, isitishe urutubishaji wote wa uraniamu, na kutoa ahadi ya kudumu ya kutotafuta kamwe silaha za nyuklia, chaneli hiyo imeripoti.
Aidha, Tehran itatakiwa kusimamisha kuyafadhili na kuyapa silaha makundi washirika katika eneo hilo na kuhakikisha kwamba Mlango-Bahari wa Hormuz unabaki wazi kwa meli za kimataifa, chaneli hiyo imesema, ikiongeza kwamba katika kubadilishana, Washington inatoa unafuu kamili wa vikwazo, usaidizi katika kuendeleza mradi wa nishati ya nyuklia kwa ajili ya matumizi ya kiraia katika eneo la Bushehr kusini mwa Iran, na kuondolewa kwa tishio la utaratibu wa "kurejesha tena" unaowezesha kurejeshwa kwa vikwazo vilivyoondolewa hapo awali vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran.
Kwa sasa, hakuna dalili kwamba vita hivyo vitaisha hivi karibuni. Ikulu ya White House imesema Jumanne kwamba huku diplomasia ikiendelea, mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran yalikuwa yakiendelea.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



