Lugha Nyingine
Afrika Kusini yasema usambazaji wa mafuta ni tulivu licha ya akiba ndogo, yaonya kuhusu kupanda kwa bei.

Bei za mafuta zikionyeshwa kwenye kituo cha mafuta jijini Johannesburg, Afrika Kusini, Machi 25, 2026. (Xinhua/Chen Wei)
JOHANNESBURG - Afrika Kusini inasambaza mafuta kwa kutosha licha ya wasiwasi kuhusu uwezekano wa upungufu unaohusishwa na mivutano katika eneo la Mashariki ya Kati, maafisa wamesema jana Jumatano, wakati huohuo wakionya kwamba mgogoro wa muda mrefu unaweza kuweka shinikizo kwenye upatikanaji na bei katika miezi ijayo.
Wakizungumza kwenye mkutano na vyombo vya habari wa mtandaoni, maafisa kutoka Wizara ya Rasilimali za Madini na Petroli ya Afrika Kusini (DMPR) na Jumuiya ya Sekta ya Mafuta ya Afrika Kusini wamesema nchi hiyo kwa sasa ina mapipa takriban milioni 8 ya mafuta ghafi katika akiba ya kimkakati - sawa na mafuta kwa wiki takriban mbili – ikiwa imeshuka sana kutoka uwezo wa kuhifadhi mapipa takriban milioni 45 kufuatia mauzo ya akiba mwaka 2016 na 2022.
Hata hivyo, hakukuwa na sababu ya haraka ya tahadhari, yamesema mashirika hayo, yakibainisha kuwa nchi hiyo inaagiza chini ya asilimia 70 ya mafuta yake kutoka Mashariki ya Kati, huku mafuta mengine ya ziada yakitoka nchi kama vile Angola na Nigeria, hali ambayo imechangia njia mbalimbali za usambazaji.
"Kama tunavyosema kwa sasa, hatugusi hata akiba hiyo ya kimkakati kwa sababu kuna mafuta mengi yanayopatikana kwenye soko la kimataifa, nje ya Mashariki ya Kati, ambayo yanakuja nchini," amesema Robert Maake, mkurugenzi wa Mfumo wa Bei ya Mafuta katika DMPR.
Hata hivyo, maafisa hao wameonya kwamba mgogoro huo unaoendelea unaweza kutishia utulivu wa usambazaji kama utaendelea, hasa kwa kuwa masoko ya mafuta duniani yanaendelea kuwa tete.
Maake amesema Afrika Kusini ina uwezekano wa kupitia ongezeko kubwa la bei ya mafuta mwezi Aprili, sawa na ongezeko lililorekodiwa Februari 2022 kufuatia kuzuka kwa mgogoro kati ya Russia na Ukraine.
Ameongeza kuwa hakuna hatua mahsusi za serikali za kulinda watumiaji kutokana na ongezeko hilo tarajiwa ambazo zimeshathibitishwa.
Huku bei za petroli huenda zitapanda hadi randi 6 (dola za Marekani karibu 0.36) kwa lita na dizeli kwa hadi randi 10 (dola za Marekani karibu 0.59) kwa lita, gharama za usafiri na chakula zinatarajiwa kuongezeka, huku waendeshaji wa huduma za teksi za mabasi madogo tayari wakiashiria uwezekano wa kupanda kwa nauli.
Wakati huo huo, ongezeko la mahitaji ya dizeli, hasa katika sekta ya kilimo, limesababisha "uhaba wa hapa na pale" katika baadhi ya maeneo. Afisa mtendaji mkuu wa AgriSA Johann Kotze ameliambia Shirika la Habari la Chian, Xinhua kwamba ununuzi wa mshituko umechangia uhaba kiasi wa usambazaji katika maeneo husika, hasa katika majimbo ya Western Cape na Eastern Cape.
Akibainisha kuwa suala kubwa zaidi ni hali ya kutokuwa na uhakika, Kotze ameonya kwamba ongezeko tarajiwa la bei ya dizeli linaweza kuwa na athari kubwa kwa uzalishaji wa kilimo na usalama wa chakula.

Bei za mafuta zikionyeshwa kwenye kituo cha mafuta jijini Johannesburg, Afrika Kusini, Machi 25, 2026. (Xinhua/Chen Wei)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



