Umoja wa Mataifa wapitisha azimio la kutangaza biashara haramu na utumwa wa Waafrika kuwa"uhalifu mkubwa dhidi ya ubinadamu"

(CRI Online) Machi 27, 2026

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) limepitisha Jumatano wiki hii rasimu ya azimio la "Kutangaza Biashara Haramu ya Utumwa wa Waafrika na Umiliki wa Waafrika Watumwa kwa Msingi wa Rangi kuwa Uhalifu Mbaya Zaidi dhidi ya Ubinadamu."

Rasimu ya azimio hilo imepitishwa kwa kura 123 za ndiyo, kura 52 zilizojizuia kupiga na tatu zilizopinga. Argentina, Israel na Marekani zilipiga kura ya kupinga.

Azimio hilo lililowasilishwa na Ghana kwa niaba ya Afrika, linatangaza kuwa "biashara haramu ya utumwa wa Waafrika na umiliki wa Waafrika watumwa kwa msingi wa rangi ni uhalifu mkubwa zaidi dhidi ya ubinadamu”, na linasisitiza "umuhimu wa kushughulikia makosa hayo ya kihistoria yanayoathiri Waafrika na watu wenye asili ya Afrika kwa njia inayohimiza haki, haki za binadamu, utu na uponyaji, na linasisitiza kwamba madai ya fidia yanawakilisha hatua madhubuti kuelekea kurekebisha makosa hayo ya kihistoria dhidi ya Waafrika na watu wa asili ya Afrika."

Baada ya kupitishwa kwa azimio hilo Waziri wa mambo ya nje wa Ghana, Bw. Samuel Okudzeto Ablakwa, aliwaambia wanahabari, kuwa jumuiya ya kimataifa imechukua hatua muhimu, ya kuzingatia na ya kihistoria kwa kupitisha azimio hilo muhimu.

(Wahariri wa tovuti:Zhao Jian)

Picha