Lugha Nyingine
OECD yakadiria ongezeko la uchumi wa Dunia kufikia asilimia 2.9 mwaka 2026 kutokana na hali wasiwasi ya Mashariki ya Kati

Picha hii iliyopigwa Machi 26, 2026 ikionyesha mwonekano wa nje ya makao makuu ya Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD), Paris, Ufaransa. (Xinhua/Wu Huiwo)
PARIS - Katika "Mtazamo Kwa Uchumi" uliotolewa jana Alhamisi, Shirika la Ushirikiano na Maendeleo ya Kiuchumi limekadiria kuwa, ongezeko la uchumi wa Dunia litapungua hadi asilimia 2.9 mwaka 2026 kutoka asilimia 3.3 mwaka 2025, baadaye kufikia asilimia 3.0 mwaka 2027.
Ripoti hiyo imesema kwamba mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati utajaribu uhimilivu wa uchumi wa dunia nzima. Imesema, bei za juu za nishati za muda mrefu zitaongeza gharama za viwanda, kupandisha mfumuko wa bei wa watumiaji, na utaleta matokeo mabaya kwa ongezeko la uchumi.
Ripoti hiyo imesema, kabla ya kupamba moto kwa mgogoro huo, ongezeko la uchumi wa dunia lilidumisha uhimilivu wake kutokana na uwekezaji na uzalishaji mkubwa unaotegemea AI na hali nzuri ya mapato na matumizi ya fedha. Baada ya mgogoro kutokea katika eneo la Mashariki ya Kati, bei za nishati zimepanda juu, na hali imezidi kuwa ya kutokuwa na uhakika, hivyo gharama zimeongezeka na kuzuia mahitaji, na kupunguza msukumo wa awali kwa ongezeko la uchumi.
Ripoti hiyo inasema, ongezeko la uchumi wa Marekani litapungua kutoka asilimia 2.0 mwaka 2026 hadi asilimia 1.7 mwaka 2027, kwa sababu uwekezaji mkubwa katika AI utadorora hatua kwa hatua kutokana na ongezeko la mapato halisi na matumizi ya watumiaji. Katika eneo la euro, ongezeko la uchumi linakadiriwa kupungua hadi asilimia 0.8 mwaka 2026 kutokana na bei za juu za nishati zinazoathiri shughuli za kiuchumi, baadaye utapanda hadi asilimia 1.2 mwaka 2027 kwa kusaidiwa na matumizi makubwa zaidi katika ulinzi wa nchi.
Ripoti imesema, mfumuko wa bei katika kundi la G20 unakadiriwa kufikia asilimia 4.0 mwaka 2026 ambao utaongezeka kwa asilimia 1.2 kuliko ilivyokadiriwa hapo kabla, baadaye utapungua hadi asilimia 2.7 mwaka 2027 kutokana na kupungua kwa shinikizo la bei ya nishati. Mfumuko wa bei wa kimsingi wa nchi zilizoendelea za G20 unakadiriwa kupungua kutoka asilimia 2.6 mwaka 2026 hadi asilimia 2.3 mwaka 2027.
OECD imetoa wito wa kuwa macho katika sera. Imesema Benki Kuu zinapaswa kuhakikisha makadirio ya mfumuko wa bei yanabaki imara na kurekebisha sera inapohitajika. Pia, serikali zimehimizwa kutoa uungaji mkono mahsusi kwa familia zilizo katika mazingira magumu na kampuni zinazoweza kustawi, kulinda uendelevu wa deni, na kuongeza ufanisi wa mapato na matumizi ya fedha.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



