Lugha Nyingine
China na Pakistan zatoa mpango wa pointi tano wa kurejesha amani na utulivu katika eneo la Ghuba na Mashariki ya Kati
BEIJING - China na Pakistan zimetoa mpango wa pointi tano wa kurejesha amani na utulivu katika eneo la Ghuba na Mashariki ya Kati wakati wa mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi na Naibu Waziri Mkuu na waziri wa mambo ya nje wa Pakistan Mohammad Ishaq Dar mjini Beijing jana Jumanne.
Wang, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), na Dar walifanya mapitio ya hali katika eneo la Ghuba na Mashariki ya Kati wakati wa mazungumzo yao.
Pande hizo mbili zimetoa yafuatayo:
Kwanza, kukomeshwa mara moja kwa uhasama: China na Pakistan zimetoa wito wa kukomeshwa mara moja kwa uhasama na kuongeza juhudi za kuzuia mgogoro huo kuenea. Msaada wa kibinadamu lazima uruhusiwe kufikishwa katika maeneo yote yaliyoathiriwa na vita.
Pili, Kuanza kwa mazungumzo ya amani mapema iwezekanavyo. Mamlaka ya nchi, ukamilifu wa ardhi, uhuru wa kitaifa na usalama wa Iran na nchi za eneo la Ghuba vinapaswa kulindwa. Mazungumzo na diplomasia ndiyo njia pekee inayofaa ya kutatua migogoro. China na Pakistan zinaunga mkono pande husika kuanzisha mazungumzo, huku pande zote zikijitolea kutatua migogoro kwa amani, na kujiepusha na matumizi au vitisho vya matumizi ya nguvu wakati wa mazungumzo hayo.
Tatu, usalama wa malengo yasiyo ya kijeshi. Kanuni ya kulinda raia katika migogoro ya kijeshi inapaswa kuzingatiwa. China na Pakistan zimetoa wito kwa pande husika kusitisha mara moja mashambulizi dhidi ya raia na malengo yasiyo ya kijeshi, kufuata kikamilifu Sheria ya Kimataifa ya Kibinadamu, na kuacha kushambulia miundombinu muhimu, ikiwemo ya nishati, ya kuondoa chumvi kwenye maji na vituo vya kuzalisha umeme, pamoja na miundombinu ya nyuklia ya amani kama vile mitambo ya kuzalisha umeme kwa nishati ya nyuklia.
Nne, usalama wa njia za usafirishaji baharini. Mlango Bahari wa Hormuz, pamoja na maji yanayozunguka, ni njia muhimu ya kimataifa ya usafirishaji wa bidhaa na nishati. China na Pakistan zimetoa wito kwa pande hizo kulinda usalama wa meli na wafanyakazi wao waliokwama katika Mlango Bahari wa Hormuz, kuruhusu kupita kwa haraka na kwa usalama kwa meli za kiraia na za kibiashara, na kurejesha hali ya kawaida ya usafirishaji kupitia Mlango Bahari wa Hormuz mapema iwezekanavyo.
Tano, kipaumbele cha Katiba ya Umoja wa Mataifa. China na Pakistan zimetoa wito wa kuimarisha utekelezaji wa ushirikiano wa kweli wa pande nyingi, kuimarisha nafasi ya Umoja wa Mataifa, na kuunga mkono kufikiwa kwa makubaliano ya kuanzisha mfumo jumuishi wa amani na kufanikisha amani ya kudumu kwa kuzingatia madhumuni na kanuni za Katiba ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



