Lugha Nyingine
Ghana yaapa kuongoza utekelezaji wa azimio la UN juu ya haki ya fidia kwa biashara ya watumwa ya Bahari ya Atlantiki

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana Samuel Okudzeto Ablakwa akitoa hotuba kwenye mkutano na waandishi wa habari juu ya kupitishwa kwa mafanikio kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa Azimio la kihistoria No. A/80/L.48 linaloongozwa na Ghana, huko Accra, Ghana, Machi 31, 2026. (Picha na Seth/Xinhua)
ACCRA - Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana Samuel Okudzeto Ablakwa ameahidi kwamba Ghana itaongoza mazungumzo endelevu duniani ili kuhimiza utekelezaji wa Azimio la Umoja wa Mataifa (UN) juu ya haki ya kutoa fidia kwa Afrika na watu wenye asili ya Afrika kutokana na athari ya biashara ya watumwa ya Bahari ya Atlantiki.
Ablakwa ametoa ahadi hiyo jana Jumanne kwenye mkutano na waandishi wa habari juu ya kupitishwa kwa mafanikio kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa Azimio la kihistoria No. A/80/L.48 linaloongozwa na Ghana, mjini Accra, Ghana, ambalo limeitangaza biashara haramu ya watumwa ya Bahari ya Atlantiki na utaratibu wa watumwa Waafrika ni uhalifu mkubwa zaidi dhidi ya ubinadamu” likiungwa mkono na nchi wanachama 123.
Waziri huyo amesema kupitishwa kwa azimio hilo bado ni mwanzo muhimu tu wa kutimiza lengo la haki ya kutoa fidia na kushikilia imani ya milele kwamba “Uhuru ni haki ya asili ya kuzaliwa ya wanaume wote na wanawake wote.”
Amesisitiza kwamba chini ya uongozi wa Rais John Dramani Mahama, Ghana ikiwa ni Mtetezi wa Umoja wa Afrika (AU) juu ya Fidia, itaendelea kufanya kazi kwa dhamira thabiti, na kuanzisha mfumo na utaratibu wa lazima kwa ajili ya kuunga mkono utekelezaji wa azimio hilo la kimataifa.
"Serikali inasisitiza zaidi kujitolea kwake kufanya kazi pamoja na nchi wanachama (wa Umoja wa Mataifa na AU) na washirika wake, kudumisha juhudi za utendaji na kusukuma mbele mazungumzo duniani juu ya haki ya kihistoria, usawa, na kutambua vya kutosha maarifa ya kihistoria waliyoyapata Waafrika na watu wenye asili ya Afrika," waziri huyo amesisitiza.
Ablakwa amezihimiza nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, "zikiwemo zile zote zilizokosa fursa ya kupigia kura azimio hilo," kujiunga na muungano huo ili kushinikiza kubomolewa kwa miundo ya ubaguzi na ubaguzi wa rangi duniani kote.
Azimio hilo linaloongozwa na Ghana na AU lililopitishwa Jumatano wiki iliyopita linatoa wito wa kuomba radhi rasmi, kurejesha mali, kulipwa fidia, kurejeshwa kwa mabaki ya kale ya kitamaduni, na kufanya marekebisho ya sera ili kukabiliana na hali ya ukosefu wa usawa wa hivi leo unaohusika na mali ya urithi wa utaratibu wa watumwa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



