Lugha Nyingine
Kenya yalenga ushirikiano wa kina zaidi na China kwenye tamasha la filamu la Kalasha linalomalizika leo
Maafisa kwenye Tamasha la Kimataifa la Filamu na Televisheni la Kalasha lililoanza Jumanne wiki hii mjini Nairobi, wamesisitiza ushirikiano unaokua na China wakati huu ambapo wanahuisha dhamira ya kuunga mkono uchumi bunifu na kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa vijana.
Likiwa ni kusanyiko kubwa la wadau muhimu katika sekta ya ubunifu ya ndani, kikanda, na kimataifa, tamasha hilo la mwaka huu litafikia mwisho leo Alhamisi na limefanyika chini ya kaulimbiu ya "Kuvumbua Jadi: Kubuni Upya Simulizi za Hadithi Moja baada ya Nyingine."
Maafisa wa Kenya na viongozi wa sekta hiyo wamesisitiza ushirikiano unaokua na China kuwa ni kichocheo muhimu cha upanuzi wa sekta bunifu ya nchi hiyo.
Waziri wa Masuala ya Vijana, Uchumi Bunifu na Michezo Salim Mvurya amesema tamasha la filamu, ambalo litafikia kilele kwa utoaji wa tuzo bora za filamu keshokutwa Jumamosi, litaimarisha nafasi ya Kenya ya kuwa kitovu cha sanaa ya maonesho.
Amebainisha kuwa ukuaji wa uchumi bunifu utategemea kutungwa kwa sera zinazoangalia mbele, uwekezaji wa kimkakati katika vifaa vya kisasa, na kunoa ujuzi wa nguvu kazi.
Timothy Owase, afisa mtendaji mkuu wa Bodi ya Filamu ya Kenya, amekaribisha ushiriki wa kampuni za China kama vile Televisheni ya Kimataifa ya Hunan katika tamasha hilo, akisema inaweza kufungua milango ya ushirikiano wa kina kati ya Kenya na China katika uchumi bunifu.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



