Lugha Nyingine
China na Australia zinapaswa kulinda kwa pamoja mfumo wa ushirikiano wa pande nyingi: Wang Yi

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), akifanya mazungumzo ya nane ya kidiplomasia na kimkakati kati ya China na Australia pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia Penny Wong, Beijing, mji mkuu wa China, Aprili 29, 2026. (Xinhua/Liu Bin)
BEIJING - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amesema jumatano kwamba China na Australia zinapaswa kusimama kwa pamoja upande sahihi wa historia na upande wa mfumo wa ushirikiano wa pande nyingi, kulinda kwa pamoja mfumo wa biashara huria duniani na kudumisha utulivu na uendeshaji mzuri wa minyororo ya viwanda na usambazaji, kuchukua jukumu la kiujenzi katika utatuzi wa kisiasa wa masuala tete ya kimataifa, na kuhimiza ujenzi wa mfumo wa usimamizi wa dunia ulio na haki na usawa zaidi.
Wang, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) ameyasema hayo Jumatano wakati alipofanya mazungumzo ya nane ya kidiplomasia na kimkakati kati ya China na Australia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia Penny Wong mjini Beijing.
Wang amesema kwamba mawasiliano ya watu na watu kati ya China na Australia yanahudumia maslahi ya pande zote mbili, na serikali zote mbili zinapaswa kuimarisha uelewano zaidi. Ameeleza matumaini yake kuwa Australia italinda usalama pamoja na haki na maslahi halali ya watu wa China.
Wang amesema ushirikiano wa kirafiki kati ya China na nchi za Visiwa vya Pasifiki haulengi upande wowote wa tatu, na Australia inapaswa kuliona hilo kwa mtazamo sahihi na wa busara.
Wang ameongeza kuwa ikiwa mwenyekiti wa zamu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia-Pasifiki (APEC), China ina nia ya kuimarisha ushirikiano na pande zote, ikiwemo Australia, ili kuendeleza mchakato wa kujenga jumuiya ya Asia-Pasifiki.
Wang pia ametoa ufafanuzi wa kina wa msimamo wa China juu ya suala la Taiwan.
Kwa upande wake, Wong amesema kwamba Australia inazingatia sera ya kuwepo kwa China moja, inapinga "kujitenga kwa Taiwan," na inatumai kwamba suala la Taiwan linaweza kutatuliwa kwa njia ya amani.
"Uchumi wa Australia na China unakamilishana kwa kiwango kikubwa, na ushirikiano wa karibu katika nyanja mbalimbali kama vile uchumi na biashara ni kwa maslahi ya pande zote mbili," amesema waziri huyo wa mambo ya nje wa Australia, akiongeza kuwa Australia inaunga mkono China katika kuandaa Mkutano wa Viongozi wa Kiuchumi wa APEC, haitengi nchi yoyote katika ushirikiano kwa ajili ya maendeleo ya nchi za visiwa, na inapenda kushirikiana na China kulinda kanuni za kimataifa na kuhakikisha usalama wa nishati.

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), akifanya mazungumzo ya nane ya kidiplomasia na kimkakati kati ya China na Australia pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia Penny Wong, mjini Beijing, mji mkuu wa China, Aprili 29, 2026. (Xinhua/Liu Bin)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



