Lugha Nyingine
Rubio asema operesheni ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Iran "imekwisha"

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House, Washington, D.C., Marekani, Mei 5, 2026. (Picha na Li Yuanqing/Xinhua)
WASHINGTON - Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio amesema kampeni ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Iran, ambayo ilianzishwa kwa pamoja na Israeli Februari 28, "imekwisha."
"Operesheni imekwisha, Epic Fury, akiwa rais alivyoliarifu Bunge. Tumemalizana na hatua hiyo," Rubio amesema juzi Jumanne kwenye mkutano na waandishi wa habari wa Ikulu ya White House.
"Sasa tuko kwenye hiki Mradi Uhuru (Project Freedom)," operesheni ya kijeshi ambayo Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon iliianzisha Jumatatu wiki hii kuongoza meli za kibiashara zilizokwama kutoka kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz, Rubio amesema, akibainisha kuwa kipaumbele cha Washington sasa ni kufungua tena njia hiyo muhimu ya maji ya kusafirishia nishati duniani.
Tangazo hilo linaonekana kuwa jaribio la utawala wa Trump la kukwepa Azimio la Mamlaka ya Vita, ambalo linamtaka rais kutafuta idhini ya bunge kuendelea na uhasama wa kijeshi baada ya siku 60.
Rubio amerudia madai ya Rais wa Marekani Donald Trump kwamba sheria ya 1973 inayoweka vikomo vya mamlaka ya rais ya vita "ni kinyume cha katiba kwa asilimia 100."
Utawala wa Trump uliliarifu Bunge wiki iliyopita kwamba uhasama dhidi ya Iran "ulikuwa umesitishwa" ilipofikia muda wa kikomo kisheria wa siku 60.
Hata hivyo, Trump hajatupilia mbali uwezekano wa kurudia mashambulizi ya kijeshi wakati huu ambapo mazungumzo yamekwama. Rubio amesema kwamba Iran sasa ina fursa ya "kuweka dhahiri" kwamba hawataki silaha ya nyuklia, jambo ambalo amesema ni muhimu kwa makubaliano ya amani na Washington.
Iran "itaishikilia dunia mateka" kwa silaha ya nyuklia, Rubio ameonya, akiishutumu Tehran kwa kujaribu kutengeneza "makombora ya kurushwa kwa masafa marefu" na kujenga vituo vya ardhini kwa ajili ya shughuli za kurutubisha uraniamu.
"Mtu fulani inabidi afanye jambo kuhusu hilo," amesisitiza.
Mapema Jumanne, Trump alikataa kueleza kile ambacho kitamaanisha kuwa ukiukaji wa makubaliano dhaifu ya kusimamisha mapigano na Iran, akisisitiza kwamba Tehran inataka makubaliano ya amani na Washington.
Februari 28, Marekani na Israeli zilianzisha mashambulizi ya pamoja dhidi ya Tehran na miji mingine ya Iran, yakimuua Kiongozi Mwandamizi wa Iran wa wakati huo Ali Khamenei, makamanda waandamizi, na raia. Iran ilijibu kwa mashambulizi mfululizo ya makombora na droni dhidi ya maeneo lengwa ya Israeli na Marekani katika nchi mbalimbali za Mashariki ya Kati, na kuimarisha udhibiti wa Mlango-Bahari wa Hormuz.
Makubaliano ya kusimamisha mapigano yalianza Aprili 8, yakifuatiwa na mazungumzo kati ya wajumbe wa Iran na Marekani mjini Islamabad ambayo yalimalizika bila makubaliano.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House, Washington, D.C., Marekani, Mei 5, 2026. (Picha na Li Yuanqing/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



