Iran yasema Marekani imeshambulia meli na maeneo ya kiraia ya Iran

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 08, 2026

TEHRAN - Kamandi kuu ya kijeshi ya Iran, Makao Makuu ya Khatam al-Anbiya, imesema jana Alhamisi usiku kwamba jeshi la Marekani limeshambulia meli mbili za Iran karibu na Mlango-Bahari wa Hormuz na kwa wakati huohuo lilifanya mashambulizi ya anga katika maeneo ya kiraia katika jimbo la kusini mwa Iran la Hormozgan na Kisiwa cha Qeshm kwa ushirikiano na baadhi ya nchi za kikanda.

Mashambulizi hayo ya jeshi "chokozi na la kigaidi" la Marekani yamekiuka makubaliano ya kusimamisha mapigano kati ya Iran na Marekani, amesema Ebrahim Zolfaghari, msemaji wa makao makuu hayo, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Iran.

"Moja ya meli hizo zilizolengwa ni meli ya mafuta iliyokuwa ikisafiri kutoka maji ya eneo la Iran karibu na Jask kuelekea Mlango-Bahari wa Hormuz, na nyingine ilikuwa ikiingia kwenye njia ya maji karibu na Fujairah katika Falme za Kiarabu," Zolfaghari amesema, akiongeza kuwa maeneo yaliyolengwa ya kiraia ni Bandar-e Khamir na Sirik, yote yako katika jimbo la Hormozgan.

Amebainisha kuwa vikosi vya jeshi la Iran vimelipiza kisasi mara moja kwa kushambulia meli za kijeshi za Marekani mashariki mwa Mlango-Bahari wa Hormuz na kusini mwa bandari ya Chabahar ya Iran, na kuzisababishia uharibifu mkubwa.

Amesema Marekani na nchi zinazoiunga mkono zinapaswa kujua kwamba Iran itatoa jibu kali kwa uchokozi wowote bila kusita.

Vyombo vya habari vya Iran vimeripoti siku hiyo ya Alhamisi usiku milipuko kadhaa katika miji ya kusini mwa Iran na mji mkuu Tehran.

Shirika rasmi la habari la Iran, IRNA limeripoti kwamba sauti mbili kubwa za milipuko zilisikika magharibi mwa Tehran, zikifuatiwa na kuanzishwa kwa ulinzi wa anga kwa dakika kadhaa.

Shirika la habari la Mehr linalomilikiwa kwa sehemu na Serikali ya Iran, limeripoti shambulio la Marekani na Israeli kwenye kambi ya kikosi cha majini katika Kaunti ya Minab katika jimbo la Hormozgan mapema leo Ijumaa.

Limemnukuu Gavana wa Minab Mohammad Radmehr akisema kwamba hakuna mtu aliyeuawa au kujeruhiwa katika shambulio hilo.

Iran, Marekani, na Israeli zilifikia makubaliano ya kusimamisha mapigano Aprili 8 baada ya siku 40 za mapigano yaliyoanza kwa mashambulizi ya Marekani na Israeli Februari 28.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha