Rais wa DRC asema uchaguzi wa 2028 huenda usifanyike iwapo vita vitaendelea mashariki mwa nchi hiyo

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 08, 2026

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Felix Tshisekedi akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Kinshasa, mji mkuu wa DRC, Mei 6, 2026. (Ikulu ya DRC/kupitia Xinhua)

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Felix Tshisekedi akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Kinshasa, mji mkuu wa DRC, Mei 6, 2026. (Ikulu ya DRC/kupitia Xinhua)

KINSHASA - Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Felix Tshisekedi amesema kwamba nchi hiyo huenda isifanye uchaguzi wake wa urais uliopangwa kufanyika mwaka 2028 iwapo vita vitaendelea mashariki mwa nchi hiyo, akiweka usalama wa taifa kuwa kiini cha ajenda ya kisiasa ya serikali yake.

"DRC inakabiliwa na vita vya uchokozi vinavyolenga kuvuruga taasisi za serikali, kupora maliasili na kudhoofisha mamlaka ya taifa," Rais Tshisekedi ameyasema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari Jumatano wiki hii mjini Kinshasa, mji mkuu wa nchi hiyo.

Amesema kurejesha usalama, kujenga upya jeshi na kuimarisha mamlaka ya serikali katika eneo la mashariki vinaendelea kuwa vipaumbele vya juu vya serikali.

Rais Tshisekedi aliingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2019 na alichaguliwa tena mwishoni mwa mwaka 2023. Kwa mujibu wa katiba ya sasa ya DRC, muhula wake wa pili unatarajiwa kumalizika mwaka wa 2028 na uchaguzi mpya wa urais unapaswa kufanyika Desemba 2028.

Amesema DRC haitaandaa uchaguzi bila ushiriki wa majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, ambako maeneo makubwa yamedhibitiwa na kundi la waasi la Vuguvugu ya Machi 23 (M23).

"Iwapo hatutaweza kumaliza vita hivi, kwa bahati mbaya, hatutaweza kuandaa uchaguzi mwaka 2028," Rais Tshisekedi amesema, akiongeza kuwa ucheleweshaji wowote utakaojitokeza hautakuwa kwa sababu anakataa kufanya uchaguzi huo.

Katika upande wa kijeshi, Rais Tshisekedi amesema, jeshi alilorithi lilikuwa limedhoofishwa na miaka mingi ya kukosa mpangilio, upungufu wa vifaa pamoja na kupenyezwa kwa makundi yenye silaha.

Rais huyo amesema serikali yake imeongeza rasilimali kwa ajili ya sekta ya ulinzi huku ikiendelea na mageuzi ya kuimarisha vikosi vya jeshi.

Amesema kwamba mazungumzo bado ni muhimu ili kumaliza mgogoro huo uliodumu kwa miongo kadhaa, akiongeza kwamba suluhisho lolote lazima lihakikishe kusitishwa kwa uungaji mkono wa makundi yenye silaha pamoja na kurejeshwa kwa mamlaka kamili ya serikali.

Hali ya usalama mashariki mwa DRC imezorota sana tangu Januari 2025. Kundi la waasi la M23 limekuwa likifanya mashambulizi ya mara kwa mara katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, likidhibiti miji kadhaa muhimu na kusababisha idadi kubwa ya vifo na majeruhi kwa raia na watu wengi kulazimika kukimbia makazi yao.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Felix Tshisekedi akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Kinshasa, mji mkuu wa DRC, Mei 6, 2026. (Ikulu ya DRC/kupitia Xinhua)

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Felix Tshisekedi akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Kinshasa, mji mkuu wa DRC, Mei 6, 2026. (Ikulu ya DRC/kupitia Xinhua)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha