Mswada wa pendekezo la Iran kwa Marekani yataka kukomeshwa vita, kuondolewa vikwazo na kizuizi cha majini

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 11, 2026

Watu wakishiriki kwenye maandamano mjini Tehran, Iran, Aprili 29, 2026. (Xinhua/Shadati)

Watu wakishiriki kwenye maandamano mjini Tehran, Iran, Aprili 29, 2026. (Xinhua/Shadati)

TEHRAN - Mswada mpya wa pendekezo la Iran kwa mazungumzo na Marekani unatoa wito wa kukomeshwa mara moja kwa mgogoro katika pande zote, kutoa hakikisho la kutorudiwa kwa "uchokozi" dhidi ya Iran, na kuondolewa kwa vikwazo vya Marekani na kizuizi cha majini, shirika la habari la Tasnim la Iran limeripoti jana Jumapili.

"Pendekezo hilo linasisitiza umuhimu wa kukomesha vita mara moja, kutoa dhamana ya kutorudiwa kwa uchokozi dhidi ya Iran, pamoja na kushughulikia masuala mengine kadhaa ndani ya mfumo wa makubaliano ya kisiasa," shirika hilo la Tasnim limemnukuu mtu anayejua kuhusu suala hilo akisema.

Pia linataka kipindi cha siku 30 kwa ajili ya kufuta vikwazo vya Marekani dhidi ya mauzo ya mafuta ya Iran, pamoja na kuachiliwa kwa mali za Iran zilizozuiliwa baada ya kufikiwa kwa makubaliano ya awali, shirika hilo limeripoti.

Marekani na Israel zilifanya mashambulizi ya pamoja dhidi ya Tehran na miji mingine ya Iran Februari 28, yakiwaua Kiongozi Mkuu wa Iran wa wakati huo Ali Khamenei, maafisa waandanmizi wa Iran na raia. Iran ilijibu kwa mashambulizi ya makombora na droni dhidi ya Israeli na maslahi ya Marekani katika eneo hilo na kuimarisha udhibiti wa Mlango-Bahari wa Hormuz.

Makubaliano ya kusimamisha mapigano kati ya pande zinazopigana yalianza kutekelezwa rasmi Aprili 8, yakifuatiwa na mazungumzo kati ya wajumbe wa Iran na Marekani mjini Islamabad, Pakistan Aprili 11 na 12, ambayo yalimalizika bila kufikiwa kwa makubaliano. Baadaye, Marekani iliweka kizuizi chake katika mlango-bahari huo wa Hormuz.

Katika wiki zilizopita, pande hizo mbili zimeripotiwa kubadilishana mipango kadhaa kupitia Pakistan, ikielezea masharti ya kumaliza mgogoro huo.

Mapema jana Jumapili, shirika rasmi la habari la Iran, IRNA liliripoti kwamba jibu la Iran kwa pendekezo la hivi punde la Marekani lilitumwa Pakistan. Jana jioni, Rais wa Marekani Donald Trump aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social kwamba jibu hilo "halikubaliki kabisa."

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha