Lugha Nyingine
Rais Xi afanya mazungumzo na Trump mjini Beijing

Rais wa China Xi Jinping akifanya mazungumzo na Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye yuko katika ziara ya kiserikali nchini China, kwenye Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing, Mei 14, 2026. (Xinhua/Ding Lin)
BEIJING - Rais wa China Xi Jinping amefanya mazungumzo na Rais wa Marekani Donald Trump aliyeko ziarani nchini China kwenye Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing jana Alhamisi, akisema kwamba mabadiliko ambayo hayajapata kuonekana katika miaka mia moja iliyopita yanaongezeka kasi kote duniani, na mabadiliko na misukosuko vinachanganyikana katika hali ya kimataifa.
"Je, China na Marekani zinaweza kuvuka Mtego wa Thucydides na kuanzisha mfano mpya wa uhusiano kati ya nchi kubwa? Je, zinaweza kukabiliana kwa pamoja na changamoto duniani na kutoa utulivu mkubwa zaidi kwa dunia? Je, zinaweza kujenga kwa pamoja mustakabali mzuri wa uhusiano wa nchi hizo mbili kwa ajili ya ustawi wa watu wa nchi zetu mbili na mustakabali wa binadamu? Haya ndiyo maswali muhimu kwa historia, kwa dunia na kwa watu," amesema Xi.
Ameongeza kuwa, ni maswali ya zama zetu ambayo viongozi wa nchi kubwa wanahitaji kuyajibu pamoja.
"Ninatarajia kushirikiana nawe katika kushika usukani na kuongoza meli kubwa ya uhusiano kati ya China na Marekani, na kufanya juhudi za kuufanya mwaka wa 2026 kuwa mwaka wa kihistoria, na kinara unaofungua ukurasa mpya wa uhusiano kati ya China na Marekani," amesema.
"Nimekubaliana na Rais Trump juu ya matarajio mapya ya kujenga uhusiano wa kiujenzi wenye utulivu wa kimkakati kati ya China na Marekani," Rais Xi amesema.
Amesema matarajio hayo mapya yatatoa mwongozo wa kimkakati kwa uhusiano wa pande mbili katika miaka mitatu ijayo na zaidi, na yanaaminikika kukaribishwa na watu wa nchi zote mbili na jumuiya ya kimataifa.
Amesema "utulivu wa kimkakati wa kiujenzi" unatakiwa kuwa ni utulivu wa kuhimiza juhudi kuu za ushirikiano, ni utulivu mzuri wenye ushindani wa kiasi cha kufaa, ni utulivu unaoendelea siku hadi siku unaoweza kusimamia migongano, na ni utulivu wa kudumu unaofuata ahadi za amani.
Rais Xi amesisitiza kwamba suala la Taiwan ni suala muhimu zaidi katika uhusiano kati ya China na Marekani.
"Kama litashughulikiwa vizuri, uhusiano wa nchi mbili utadumisha utulivu kwa ujumla. Vinginevyo, nchi hizi mbili zitakuwa na migongano na hata migogoro, na kuupelekea uhusiano mzima katika hali hatari sana," Rais Xi amesema, akihimiza upande wa Marekani kuwa na uangalifu zaidi katika kushughulikia suala hilo la Taiwan.
Kwa upande wake, Rais Trump amesema ni heshima kubwa kufanya ziara ya kiserikali nchini China, akimwita Xi kiongozi mzuri na China nchi nzuri. "Ninamheshimu sana Rais Xi na kuwaheshimu watu wa China," Rais Trump amesema.
Ameeleza nia yake ya kushirikiana na Rais Xi katika kuimarisha mawasiliano na ushirikiano, kushughulikia migongano kwa kufaa, kuanzisha uhusiano wa pande mbili kuwa bora zaidi katika historia yake, na kujenga siku nzuri zaidi za baadaye za nchi hizo mbili.
Marekani na China ni nchi muhimu na zenye nguvu zaidi duniani, na nchi hizo mbili zikishirikiana zitaweza "kufanya mambo mengi makubwa na mazuri kwa ajili ya nchi hizo mbili na dunia," amesema.
Rais Trump amewahimiza wajumbe wa wanaviwanda na wafanyabiashara wa Marekani kupanua ushirikiano na China.
Marais hao wawili wamebadilishana maoni juu ya masuala makubwa ya kimataifa na kikanda, kama vile hali ya Mashariki ya Kati, mgogoro wa Ukraine, na Peninsula ya Korea.
Pia wamekubaliana kuungana mkono katika kuandaa Mkutano wa Viongozi wa Uchumi wa APEC na Mkutano wa G20 mwaka huu.

Rais wa China Xi Jinping akifanya mazungumzo na Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye yuko katika ziara ya kiserikali nchini China, kwenye Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing, Mei 14, 2026. (Xinhua/Ding Lin)

Rais wa China Xi Jinping akifanya mazungumzo na Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye yuko katika ziara ya kiserikali nchini China, kwenye Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing Mei 14, 2026. (Xinhua/Ding Lin)

Rais wa China Xi Jinping akifanya mazungumzo na Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye yuko katika ziara ya kiserikali nchini China, kwenye Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing Mei 14, 2026. (Xinhua/Yin Bogu)

Rais wa China Xi Jinping akifanya mazungumzo na Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye yuko katika ziara ya kiserikali nchini China, kwenye Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing Mei 14, 2026. (Xinhua/Li Xiang)

Rais wa China Xi Jinping akifanya mazungumzo na Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye yuko katika ziara ya kiserikali nchini China, kwenye Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing Mei 14, 2026. (Picha na Xiao Yi/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



