Lugha Nyingine
Viongozi wa AU na UN walaani uingiliaji wa nje katika msukosuko wa usalama wa Afrika
ADDIS ABABA - Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) Mahmoud Ali Youssouf na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres wameonya kwamba uingiliaji wa nje unachochea msukosuko wa usalama barani Afrika.
Viongozi hao wawili wametoa madai hayo katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari Jumatano wiki hii kwenye makao makuu ya AU mjini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, baada ya kusaini tamko jipya la kuongeza ushirikiano kati ya AU na UN.
"Misukosuko mingi ya usalama barani huchochewa kutoka nje. Rasilimali za kifedha, silaha, wakati mwingine hata wapiganaji huja kupigana vita vingine kutoka mabara mengine," Youssouf ameuambia mkutano huo na waandishi wa habari.
Amesema uingiliaji huo unakwenda kwenye kiwango cha kuvuruga michakato ya upatanishi na utatuzi, ukisababisha changamoto kubwa kwa AU na UN kushughulikia msukosuko wa usalama barani humo, ikiwemo katika Sahel, Sudan, Pembe ya Afrika na mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Youssouf amesema uingiliaji huo unazihitaji AU, UN na washirika wengine kutumia juhudi zaidi kudhibiti misukosuko hiyo. "AU lazima iongoze mazungumzo yoyote ya amani barani, kwa msingi wa kanuni ya suluhu za Afrika kwa migogoro ya Afrika."
Guterres, kwa upande wake, amesema ni jambo lisilovumilika kabisa kwamba nchi ambazo ni za nje ya Afrika kuingilia migogoro ya Afrika, kutoa silaha na uungaji mkono wa kisiasa kwa lengo la kuhudumia maslahi yao ya kimkakati au kiuchumi.
"Tunapawa kuendelea kuimarisha diplomasia yetu ya pamoja, ili kuhakikisha kwamba tunaweka mazingira kwa aina hii ya uingiliaji kukoma na kwa wahusika wengine kuweza kufikia makubaliano ya kisiasa, na kuweza kumaliza migogoro hii," amesema.
Kwa mujibu wa Guterres, dunia inashuhudia aina mpya ya vita ambapo majeshi hayapigani yenyewe kwa yenyewe bali hurusha droni dhidi ya raia.
"Pia tunapaza sauti zetu, tukilaani nchi hizo zinazotoa droni ambazo hazitengenezwi barani Afrika, kwani zinasababisha kafara mbaya kwa watu wa Afrika," ameongeza.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



