Lugha Nyingine
Netanyahu na Trump wajadili uwezekano wa mapigano mapya dhidi ya Iran
Televisheni ya Kan inayomilikiwa na serikali ya Israel imeripoti kuwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais wa Marekani Donald Trump jana Jumapili walijadili kwa njia ya simu uwezekano wa mapigano mapya dhidi ya Iran.
Kituo hicho, kikimnukuu afisa mwandamizi wa Israel, kimesema Marekani inatarajiwa kufanya mashambulizi pamoja na Israel kama itaanza tena vita dhidi ya Iran.
Afisa mmoja katika serikali ya Isral ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba, baadaye jioni ya siku hiyo ya Jumapili, Netanyahu aliitisha mkutano wa baraza la mawaziri, ambapo pande mbalimbali za vita vya Israel zimejadiliwa.
Hatua hiyo inakuja baada ya Trump kudokeza kwamba Washington inaweza kuzidisha mapambano yake na Iran, akionya katika chapisho lake kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social kwamba "kwa Iran, saa zinakaribia, na ni bora waanze kuchukua hatua, haraka, vinginevyo hawakutakuwa na chochote kilichobakia."
Wakati huohuo Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amesema Marekani na Israel zimekuwa zikichonganisha mataifa ya Kiislamu kwa kuleta mgawanyiko na kutoaminiana miongoni mwao.
Kwenye mkutano wa jana Jumapili na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistani aliyekuwa ziarani nchini humo Mohsin Naqvi, Rais Pezeshkian amesema Iran inatafuta "uhusiano mzuri na wa kudumu kwa msingi wa ujirani mwema" na mataifa ya Kiislamu katika eneo la Asia Magharibi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



