Watu 4 wauawa, 30 wajeruhiwa kwenye maandamano ya kupinga ongezeko la bei ya mafuta nchini Kenya

(CRI Online) Mei 19, 2026

Kwa mujibu wa Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya Onesimus Kipchumba Murkomen, watu wanne wameuawa na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa katika sehemu mbalimbali za nchi hiyo kwenye vurugu za maandamano ya nchi nzima na mgomo mkubwa wa waendesha usafiri wa umma uliosababishwa na ongezeko kubwa la bei ya mafuta.

Akiongea na wanahabari jijini Nairobi jana Jumatatu, Murkomen amesema waandamanaji zaidi ya 300 wamekamatwa baada ya waandamanaji kuwasha moto, kufunga barabara, na kupambana na polisi.

“Polisi wameanzisha uchunguzi ili kubaini kama waliofariki walikuwa raia wasio na hatia au wahalifu waliofanya uhalifu mbalimbali.” Murkomen amesema.

Aidha amelaani matukio ya vurugu, uporaji, na uharibifu wa mali yaliyoripotiwa kwenye maandamano hayo katika maeneo hasa ya katikati mwa Kenya.

Muungano wa Sekta ya Uchukuzi wa Kenya uliitisha mgomo huo juzi Jumapili, ukisema kwamba bei kubwa ya mafuta imesukuma gharama za uendeshaji kuwa kubwa kupita kiasi. Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli ya Kenya (EPRA) iliongeza bei ya mafuta Mei 14, ambapo petroli imefikia shilingi 16.65 (dola za Marekani karibu 0.12) kwa lita na dizeli shilingi 46.29.

(Wahariri wa tovuti:Zhao Jian)

Picha