Lugha Nyingine
Waendesha shughuli za utalii wa China na Afrika watafuta ushirikiano mpya kwenye Mkutano wa Utalii wa Afrika

Watu wakitembelea eneo la maonyesho la Mkutano wa Utalii wa Afrika, Africa's Travel Indaba 2026, Durban, Afrika Kusini, Mei 12, 2026. (Xinhua/Chen Wei)
DURBAN – Waendesha shughuli za utalii wa China na Afrika wanatafuta ushirikiano na fursa mpya za biashara kwenye Mkutano wa Utalii wa Afrika 2026 (Africa's Travel Indaba 2026) uliomalizika hivi karibuni mjini Durban, Afrika Kusini wakati ambapo maeneo ya kitalii ya Afrika yakiongeza juhudi za kuvutia watalii kutoka soko linalokua la China la utalii wa kwenda nje ya nchi.
Maonyesho ya biashara ya Mei 12-14 ya mkutano huo, yaliyofanyika katika jiji la pwani la Afrika Kusini la Durban, yaliwakutanisha waonyeshaji, mashirika ya ndege, waendeshaji shughuli za utalii na maafisa kutoka nchi mbalimbali za Afrika, huku majadiliano yakijikita katika upatikanaji rahisi wa visa, bidhaa mahsusi za utalii na ushirikiano wa kina zaidi wa utalii na China.
Akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa aliuelezea utalii kuwa ni onyesho hai zuri la utambulisho wa taifa na kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi kwa nchi za Afrika.
Alitoa wito kwa nchi za Afrika kuboresha muunganisho wa kikanda na kuwezesha usafiri kwa kwenda kutalii ndani ya Afrika wakati huohuo zikipanua masoko ya kimataifa kama vile China ili kutumia vyema mchango wa utalii katika kukuza uchumi wa bara.
Maonyesho hayo ya mwaka huu yaliyofanyika chini ya kaulimbiu "Afrika Isiyo na Vizuizi: Kukuza Uchumi wa Utalii wa Afrika," yalivutia waonyeshaji bidhaa 1,225 kutoka nchi 22 za Afrika na wanunuzi karibu 1,000 kutoka nchi na maeneo zaidi ya 40.
Kwenye mabanda ya kitaifa, kampuni za utalii kutoka Namibia, Angola, Gabon, Mauritius na nchi zingine za Afrika zilitoa vivutio vyao vya kipekee, vikiwemo utalii kusafiri jangwani, utalii wa ikolojia wa misitu ya mvua na likizo za visiwani.
Akizungumza na Shirika la Habari la China, Xinhua, Waziri wa Uchumi wa Msumbiji Basilio Muhate alisema kwamba nchi hiyo inauchukulia utalii kama nguzo muhimu ya kuufanya uchumi kuwa wa kutegemea sekta mbalimbali, akibainisha kuwa Msumbiji inajivunia kilomita takriban 2,700 za pwani na rasilimali nyingi za utalii.
"Soko la China la utalii wa kwenda nje ya nchi lina uwezo mkubwa sana, na tunaweka umuhimu mkubwa kwenye ushirikiano wa utalii na China," alisema.
Gcobani Mancotywa, meneja mkuu wa kikanda kwa Asia, Australasia na Mashariki ya Kati katika Shirika la Utalii la Afrika Kusini, ameliambia Xinhua kwamba China inaendelea kuwa soko muhimu la sekta ya utalii ya Afrika Kusini.
Amesema shirika hilo limezindua akaunti rasmi kwenye majukwaa makuu ya mitandao ya kijamii ya China kama vile Xiaohongshu, Weibo na Douyin ili kuwafahamisha watalii wa China mandhari ya mazingira ya asili na uanuwai wa kitamaduni wa nchi hiyo.
Takwimu kutoka Shirika la Utalii la Afrika Kusini zinaonyesha kwamba watalii wapatao 45,000 wa China walitembelea Afrika Kusini mwaka 2025, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuzidi 50,000 mwaka huu.
Wawakilishi jumla ya 35 wa sekta ya utalii wa China walihudhuria maonyesho hayo ya mwaka huu.
Liu Yina, mwanzilishi na afisa mtendaji mkuu wa WTA Travel, kampuni ya safari za utalii yenye makao yake makuu Afrika Kusini, amesema rasilimali za kipekee za utalii za Afrika, zinazochanganya mandhari ya mazingira ya asili na mambo mengi ya kitamaduni, zinavutia idadi inayoongezeka ya watalii wa China.

Basilio Muhate, Waziri wa Uchumi wa Msumbiji, akizungumza katika mahojiano na Shirika la Habari la China, Xinhua kwenye Mkutano wa Utalii wa Afrika, Africa's Travel Indaba 2026, Durban, Afrika Kusini, Mei 12, 2026. (Xinhua/Chen Wei)

Gcobani Mancotywa, meneja mkuu wa kikanda kwa Asia, Australasia na Mashariki ya Kati katika Shirika la Utalii la Afrika Kusini, akizungumza katika mahojiano na Shirika la Habari la China, Xinhua kwenye Mkutano wa Utalii wa Afrika, Africa's Travel Indaba 2026, Durban, Afrika Kusini, Mei 12, 2026. (Xinhua/Chen Wei)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



