Lugha Nyingine
Serikali ya Botswana yaiona sera ya ushuru-sifuri ya China kuwa fursa kubwa ya kuongeza mauzo ya nje
Wizara ya Viwanda na Ujasiriamali ya Botswana imesema, China imeondoa ushuru kwa bidhaa stahiki kutoka Botswana kuanzia Mei Mosi, hatua ambayo ni fursa kubwa kwa biashara za nchi hiyo kuongeza mauzo ya nje na kutoa fursa za ajira.
Kwenye mkutano na wanahabari jana Jumanne, Wizara hiyo imesema kuondolewa kwa ushuru huo kunamaanisha bidhaa asilia za Botswana sasa zinaweza kuingia soko la China bila ya gharama za ushuru wa ziada, hali ambayo inafanya kuwa rahisi na gharama ndogo zaidi kwa wafanyabiashara wa nchini humo kuuza bidhaa zao katika moja ya masoko makubwa zaidi duniani.
Wizara hiyo imetaja baadhi ya sekta muhimu zinazohitajika, zikiwemo za bidhaa za nyama na mifugo, bidhaa za vyakula vilivyosindikwa, bidhaa za kilimo bustani, bidhaa za ngozi na vitambaa, na pia sanaa za uchongaji.
Sera hiyo ya ushuru-sifuri ya China imepanuliwa na kuhusisha nchi 53 za Afrika zenye uhusiano wa kidiplomasia na China, na ilianza kutekelezwa rasmi Mei Mosi mwaka huu.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



