DRC yapambana kudhibiti Ebola huku idadi ya vifo ikifikia 136

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 20, 2026

Roger Kamba, Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari juu ya mlipuko wa Ebola, Kinshasa, mji mkuu wa DRC, Mei 19, 2026. (Str/Xinhua)

Roger Kamba, Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari juu ya mlipuko wa Ebola, Kinshasa, mji mkuu wa DRC, Mei 19, 2026. (Str/Xinhua)

KINSHASA - Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) inapambana kudhibiti mlipuko wake wa hivi punde kabisa wa Ebola, baada ya kutangazwa Mei 15 katika jimbo la mashariki la Ituri.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari jana Jumanne mjini Kinshasa, Waziri wa Afya wa DRC Roger Kamba amesema kwamba visa 543 vinavyoshukiwa vimesharekodiwa, ikiwemo visa 32 vilivyothibitishwa maabara, huku idadi ya vifo ikifikia 136. Kamba amesema vifo hivyo ni visa vinavyoshukiwa kuhusishwa na Ebola, huku uchunguzi ukiendelea ili kubaini vile vinavyohusishwa moja kwa moja na virusi hivyo.

Huko Bunia, mji mkuu wa jimbo la Ituri, afisa wa Shirika la Afya Duniani Adelheid Marschang Ancia amesema jana Jumanne kwamba mamlaka za afya bado hazijatambua "mgonjwa wa kwanza kuambukizwa."

"Kile tunachojua kwa sasa ni kwamba Mei 5, kulikuwa na ... mtu aliyefariki Bunia," amesema, akiongeza kuwa mwili huo baadaye ulipelekwa Mongbwalu, ambapo hali ya mgusano unaohusiana na mazishi hayo unaweza kuwa umechangia maambukizi.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) Jean Kaseya alisema tarehe 16 Mei, "Mlipuko huu ulianza Aprili. Hadi sasa, hatujui chanzo cha kwanza kabisa. Inamaanisha kuwa hatujui ni kwa ukubwa wa mlipuko huu umesambaa kwa kiwango gani."

Kwa mujibu wa Kamba, matokeo ya uchunguzi wa vinasaba yaliashiria kuwa kirusi kinachosambaa kwa sasa "kimetoka msituni," akikielezea kuwa ni maambukizi mapya yanayotokana na msitu badala ya kuibuka tena kwa mnyororo wa kirusi cha zamani.

Mlipuko huo unasababishwa na virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo, aina isiyo ya kawaida sana iliyobainika kwa mara ya kwanza nchini Uganda mwaka 2007, na kisha kusababisha mlipuko katika eneo la Isiro nchini DRC mwaka 2012.

Kamba amesema ukosefu wa chanjo na matibabu maalum ni chanzo cha wasiwasi, lakini DRC ina uzoefu mkubwa katika kupambana dhidi ya Ebola. Amesema mwitikio utaweka mkazo katika utambuzi wa haraka, kutengwa kwa wagonjwa, ulinzi wa wafanyakazi wa afya na mazishi salama.

Wakati huo huo, akizungumza mjini Kinshasa jana Jumanne, Kaseya wa Africa CDC ameainisha kuwa chanjo tatu mbadala zilikuwa zikipitiwa, ikiwemo ya Ervebo.

Mlipuko huo umeibuka katika eneo ambalo tayari linakabiliwa na migogoro, watu waliokimbia makazi yao na uwezo mdogo wa huduma ya afya.

Uganda pia imethibitisha visa viwili vilivyoingizwa Kampala, ikiwemo kifo kimoja, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani. Nchi jirani, zikiwemo Rwanda, Burundi na Tanzania, zimeongeza ufuatiliaji, ukaguzi wa mipakani na hatua za utayari wa kukabiliana na dharura.

DRC imekuwa ikikabiliwa na milipuko ya mara kwa mara ya Ebola tangu virusi hivyo vilipogunduliwa kwa mara ya kwanza karibu na Mto Ebola mwaka 1976. Mlipuko wake mkubwa zaidi, uliosababishwa na kirusi aina ya Zaire, ulilikumba eneo la mashariki mwa DRC kuanzia 2018 hadi 2020, na kuua watu zaidi ya 2,200.

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha