Lugha Nyingine
Teknolojia ya Juncao ya China yabadilisha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa visiwani Zanzibar, Tanzania

Tahiya Bauso Massawe, mkulima na mfugaji wa ng’ombe wa maziwa kutoka Tanzania, akiwa amebeba nyasi freshi za Juncao zilizovunwa punde, Zanzibar, Tanzania, Mei 12, 2026. (Xinhua/Nurdin Pallangyo)
DAR ES SALAAM - Kwenye kijiji tulivu cha wakulima cha Bumbisudi katika kisiwa cha Zanzibar, Tanzania, mkulima na mfugaji wa ng’ombe wa maziwa Tahiya Bauso Massawe anatembea kupitia safu za nyasi ndefu za kijani, akipangusa mikono yake dhidi ya majani yanayoyumba taratibu katika upepo mwanana cha pwani.
Kile kilichoonekana kuwa chakula cha asili cha mifugo ya kawaida kimekuwa uti wa mgongo wa mabadiliko makubwa -- si tu kwa biashara yake ya maziwa, bali pia kwa wakulima wengi wadogo wanaotafuta njia ya kutoka katika uzalishaji mdogo na mapato yasiyo na uhakika.
Nyasi hiyo inaitwa Juncao, teknolojia iliyovumbuliwa nchini China na kuletwa Tanzania kupitia programu za ushirikiano wa kilimo. Kwa Massawe, imeleta maziwa zaidi, ajira zaidi, na imani mpya katika mustakabali wa kilimo cha vijijini.
"Kupitia mradi huu wa Juncao, tuliipanda (nyasi hiyo) kwa wingi na kulisha ng'ombe wetu. Tuliona tofauti dhahiri ikilinganishwa na nyasi za kawaida," Massawe amesema alipokuwa akihudumia kundi lake la ng’ombe wa maziwa.
Kwa miaka mingi, wafugaji kote Zanzibar walitegemea chakula cha mifigo cha jadi kama vile ukoka na pembergrass. Wakati wa kiangazi, nyasi mara nyingi hukauka, na kuwaacha wakulima wakihangaika kulisha mifugo yao na kudumisha uzalishaji wa maziwa, jambo ambalo hufanya ufugaji wa mifugo ya maziwa uwe usiotabirika na kuwanyima fedha.
Hilo lilianza kubadilika baada ya Wizara ya Kilimo, Maliasili, Umwagiliaji, na Mifugo ya Zanzibar kuanzisha teknolojia ya Juncao kwa wakulima wenyeji na kuwafunza jinsi ya kulima na kutumia nyasi kama chakula cha mifugo.
"Tuliongozwa jinsi ya kulisha nyasi hii yenye lishe ambayo inaweza kuongeza uzalishaji wa maziwa," amesema.
Leo, shamba lake linazalisha kati ya lita 100 na 120 za maziwa kila siku, karibu mara mbili ya kiasi alichokuwa akipata hapo awali kwa kutumia mifumo ya kawaida ya kulisha.
Mafanikio hayo yameenda zaidi ya mavuno ya maziwa. Shamba hilo sasa linaajiri wafanyakazi zaidi ya 16, wakiwemo wanawake na vijana wanaohusika katika kilimo cha chakula cha mifugo, ukamuaji, na usimamizi wa shamba.
Mafanikio hayo pia yameimarisha kuaminika kwa wakulima kwa taasisi za fedha.
Teknolojia hiyo ya Juncao ilivumbuliwa na mwanasayansi Mchina Lin Zhanxi wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Misitu cha Fujian katika miaka ya 1980. Mfumo huu jumuishi hutumia nyasi zilizoandaliwa maalum kwa ajili ya kilimo cha uyoga, chakula cha mifugo, urejesho wa ikolojia, na uzalishaji wa mbolea ya oganiki.
Teknolojia hiyo iliingia Tanzania kwa mara ya kwanza kupitia miradi ya majaribio ya ukuzaji wa uyoga. Utumiaji mpana ulianza baada ya mwanaikolojia wa Tanzania Elly Ligate kurudi nyumbani mwaka 2018 baada ya kukamilisha masomo ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Kilimo na Misitu cha Fujian cha China.
Mwaka 2019, Ligate alisaidia kuanzisha kitalu cha Juncao katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) mkoani Morogoro, na hivyo kutengeneza njia ya teknolojia hiyo kuenea kote Tanzania Bara na Zanzibar.
Kwa mujibu wa Ligate, sasa Watanzania zaidi ya 2,000 hulima nyasi hizo za Juncao kwa ajili ya chakula cha mifugo, huku wakulima wapatao 500 wakizitumia kama kichocheo cha uyoga.

Tahiya Bauso Massawe, mkulima na mfugaji wa ng’ombe wa maziwa kutoka Tanzania, akiwalisha ng'ombe nyasi freshi za Juncao zilizokatwa punde kwenye shamba la maziwa, Zanzibar, Tanzania, Mei 12, 2026. (Xinhua/Nurdin Pallangyo)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



