Mlipuko wa Ebola wafika Jimbo la Kivu Kusini la DRC huku visa vinavyoshukiwa vikiongezeka

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 22, 2026

Mfanyakazi wa matibabu akivinyunyizia dawa vifaa kuua vijidudu kabla ya mazishi ya mtu anayeshukiwa kufariki kwa Ebola, Bunia, Jimbo la Ituri, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mei 21, 2026. (Str/Xinhua)

KINSHASA - Mlipuko wa hivi punde wa Ebola umeenea hadi Jimbo la Kivu Kusini la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), huku wasiwasi mpya ukiibuka juu ya maambukizi mapana zaidi katika eneo lenye hali tete ya kiusalama la mashariki mwa nchi hiyo.

Jana Alhamisi, kundi la waasi la Vuguvugu la Machi 23 (M23) lilithibitisha kisa kipya mjini Bukavu, mji mkuu wa Kivu Kusini.

Kundi hilo, ambalo limekuwa likiushikilia mji huo tangu Februari 2025, limesema kwamba mwanamume mwenye umri wa miaka 28 alikuwa amesafiri kutoka Kisangani, mji mkuu wa Jimbo la Tshopo, na amefariki kabla ya vipimo vya ugonjwa wake kuthibitishwa.

Ingawa jimbo hilo la Tshopo halijashuhudia visa vyovyote hadi sasa, Mji wa Kisangani -- moja ya vituo vya usafiri vyenye pilika nyingi zaidi nchini DRC -- umeibuka kuwa eneo jipya la kufuatiliwa na kuhitaji umakini, wakati huu ambapo mamlaka zikijitahidi kubaini ni kwa kiasi gani virusi hivyo vinaweza kuwa vimeenea kabla ya kubainika.

Mlipuko huo, ulioripotiwa awali katika Jimbo la Ituri, sasa umeathiri Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, wakati huohuo visa viwili vilivyothibitishwa pia vimeripotiwa katika nchi jirani ya Uganda.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa jana Alhamisi na Waziri wa Afya wa DRC Roger Kamba, visa 626 vinavyoshukiwa na vifo 159 vinavyodhaniwa kutokana na ebola vimerekodiwa tangu nchi hiyo ilipotangaza mlipuko wake huo wa 17 tarehe 15 Mei.

Upinzani wa jamii umekuwa kikwazo kingine katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Waziri wa Afya wa DRC Roger Kamba alisema Jumanne wiki hii kwamba tahadhari hiyo imecheleweshwa ndani ya jamii zilizoathiriwa, kwani baadhi ya wakazi waliamini ugonjwa huo ulikuwa "wa kimiujiza."

Katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wake, M23 imesema kwamba sampuli zaidi ya 200 kutoka visa vinavyoshukiwa zimetumwa Goma, mji mkuu wa Kivu Kaskazini, kwa ajili ya uchambuzi wa maabara. Katika mji huo wa Goma, kisa cha mtu mmoja kilichothibitishwa bado kiko chini ya uangalizi mkali wa kimatibabu, wakati huohuo watu waliotambuliwa kuwa wamekutana naye wakiwa wametengwa, kundi hilo limeongeza.

Siku ya Alhamisi, huko Rwampara, kitovu cha mlipuko katika Jimbo la Ituri, waandishi wa habari wa Shirika la Habari la China, Xinhua waliona eneo la kutenga watu wanaoshukiwa kuambukizwa Ebola likichomwa moto baada ya mapigano katika kituo hicho.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, ameonya kwamba idadi ya visa inatarajiwa kuendelea kuongezeka, kutokana na muda ambao virusi hivyo vilionekana kuenea kabla ya mlipuko kubainika.

Kwa mujibu wa maafisa wa WHO, uchunguzi bado unaendelea ili kubaini hasa ni lini na wapi mlipuko ulianza, lakini ukubwa wa janga hilo unaonyesha kuwa virusi hivyo vinaweza kuwa vilikuwa vikisambaa kwa muda kabla ya kuthibitishwa.

WHO imeweka wazi kwamba hatari kutoka kwenye mlipuko huo imefanyiwa tathimini kuwa kubwa katika ngazi za kitaifa na kikanda, lakini ni ndogo duniani kote.

Eneo la kutengwa kwa watu wanaodhaniwa kuambukizwa Ebola likiwa limechomwa moto katika mji wa Rwampara, karibu na Bunia ya Jimbo la Ituri, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mei 21, 2026. (Str/Xinhua)

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha