Lugha Nyingine
Tamasha la Siku ya Afrika lafanyika Beijing likiangazia mabadilishano kati ya China na Afrika

Tamasha la wazi la Siku ya Afrika mwaka 2026 likifanyika mjini Beijing, China, Mei 23, 2026. (Picha na People’s Daily Online)
Tamasha la wazi la Siku ya Afrika mwaka 2026 kwa Waafrika wanaoishi China limefanyika mjini Beijing, China juzi Jumamosi likiwaleta pamoja wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi mbalimbali duniani hususani za Afrika, maofisa wa serikali ya China, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa nchini China na watu wa pande mbili za China na Afrika kusherehekea utajiri wa kitamaduni wa Afrika.
Tamasha hilo la mwaka huu ambalo ni la kwanza kufanyika kabla ya Siku ya Afrika ambayo huadhimishwa kila mwaka Mei 25, kwa mwaka huu wa 2026 linaangukia katika mwaka ambao umetangazwa rasmi kuwa Mwaka wa Mawasiliano ya Watu kati ya China na Afrika na kulifanya tukio zima kuzunguka mada hiyo kuu.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa tamasha hilo Balozi wa Burundi nchini China Telesphore Irambona ambaye pia ni mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Afrika (AU) nchini China na mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya Siku hiyo ya Afrika nchini China, amesema kwamba Siku ya Afrika ya mwaka huu ina mada kuhusu mawasiliano kati ya China na Afrika.

Balozi wa Burundi nchini China Telesphore Irambona ambaye pia ni mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Afrika (AU) nchini China na mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya Siku ya Afrika nchini China akihutubia hafla ya ufunguzi wa Tamasha la wazi la Siku ya Afrika mwaka 2026 mjini Beijing, China, Mei 23, 2026. (Picha kwa hisani ya waandaaji/kupitia People’s Daily Online)
“Huu ni wakati maalum unaoturuhusu kuingiza nguvu hai mpya katika urafiki na ushirikiano kati ya China na Afrika. Ninapenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha nyote na kusisitiza umuhimu wa wakati huu kwa ajili ya mawasiliano ya kitamaduni kati ya China na Afrika.”
Kwa upande wake Balozi wa Cameroon nchini China Martin Mpana, ambaye pia ni Mwandamizi wa Mabalozi wote nchini China, amesema kuwa tamasha hilo limeonyesha urafiki na ushirikiano unaozidi kuongezeka kati ya Afrika na China.

Balozi wa Cameroon nchini China Martin Mpana, ambaye pia ni Mwandamizi wa Mabalozi wote nchini China akihutubia hafla ya ufunguzi wa Tamasha la wazi la Siku ya Afrika mwaka 2026 mjini Beijing, China, Mei 23, 2026. (Picha kwa hisani ya waandaaji/kupitia People’s Daily Online)
“Katika mawasiliano na miingiliano ya kati ya lugha, tamaduni, na watu, tumeona uwazi, kuheshimiana, kuelewana—sifa muhimu za muda mrefu za uhusiano kati ya China na Afrika.” Amesema.
Ameeleza kwamba uhusiano kati ya Afrika na China umeendelea na kuwa wa kina zaidi katika miongo michache iliyopita, ukijengwa juu ya kuheshimiana, mshikamano na kusaidiana, maono ya pamoja, na kujitolea kwa maendeleo ya pamoja.
“Kwa miaka mingi, ushirikiano wetu umepanuka hadi maeneo mengi, ukijumuisha biashara, uwekezaji, miundombinu, elimu, sayansi na teknolojia, huduma ya afya, na maendeleo yanayotilia maanani watu.” Amebainisha, akiongeza kuwa, mawasiliano ya kitamaduni na muunganisho wa watu kwa watu daima vimekuwa nguzo imara na za kudumu zaidi za uhusiano huo.
Kwa upande wake, Li Bin, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Mambo ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya China, amesema kwamba, miaka sitini na tatu iliyopita, chini ya bendera ya Pan Afrika, Umoja wa Afrika ulianzishwa na China na Afrika katika kipindi hicho zimepigana bega kwa bega katika mapambano dhidi ya ubeberu, ukoloni na umwamba na kusonga mbele mkono kwa mkono katika njia ya maendeleo na ustawi, na kujenga uhusiano wa kindugu usiovunjika.

Li Bin, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Mambo ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya China akihutubia hafla ya ufunguzi wa Tamasha la wazi la Siku ya Afrika mwaka 2026 mjini Beijing, China, Mei 23, 2026. (Picha kwa hisani ya waandaaji/kupitia People’s Daily Online)
Ameeleza kuwa, mwaka huu ni wa maadhimisho ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Afrika, na pia ni Mwaka wa Mawasiliano ya Watu kati ya China na Afrika, uliokubaliwa kwa pamoja na Rais Xi Jinping wa China na viongozi wa Afrika.
Katika muktadha huo, amesema Tamasha hilo la Utamaduni la Siku ya Afrika halionyeshi tu tamaduni nzuri za Afrika, lakini pia linatoa jukwaa muhimu kwa China na Afrika kuendeleza kufunzana kati ya ustaarabu na kuimarisha urafiki wa kitamaduni.
“Natumai kwa dhati marafiki kutoka China na Afrika wanaweza kupata uzoefu kamili wa mvuto usio na mwisho wa ustaarabu wa kale wa China na Afrika, kugusa mdundo mmoja wa kitamaduni, na kuvuta mioyo yetu karibu zaidi.” Amesema.
Siku ya Afrika itaadhimishwa leo Mei 25 kote duniani. Ilianzishwa rasmi baada ya kuanzishwa kwa Jumuiya ya Umoja wa Nchi za Afrika (OAU) Mei 25, 1963 ambayo kwa sasa inaitwa Umoja wa Afrika (AU). Katika tamasha hilo, mambo mbalimbali ya kiutamaduni ya Afrika yalikuwa kivutio hasa maonyesho ya ngoma za jadi, mavazi na bidhaa mbalimbali za kibunifu na kitamaduni.

Watu wakihudhuria hafla ya ufunguzi wa Tamasha la wazi la Siku ya Afrika mwaka 2026 mjini Beijing, China, Mei 23, 2026. (Picha kwa hisani ya waandaaji/kupitia People’s Daily Online)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



