Lugha Nyingine
Mkuu wa WHO atoa wito wa kufikiria upya marufuku ya usafiri wakati DRC ikipambana na mlipuko wa Ebola

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus akionekana Bunia, mji mkuu wa Jimbo la Ituri katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mei 30, 2026. (Xinhua)
BUNIA, DRC - Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus ametoa wito kwa nchi ambazo zimeweka marufuku ya usafiri au kufunga mipaka ili kukabiliana na mlipuko wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Uganda kufikiria upya hatua hizo.
Akizungumza Jumamosi kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mjini Bunia, mji mkuu wa Jimbo la Ituri kaskazini mashariki mwa nchi hiyo na ambao ni eneo lililoathirika zaidi kwa Ebola, Tedros amesema vizuizi vya namna hiyo vinaweza kutatiza juhudi za kukabiliana na zinaleta hatari ya kukatisha tamaa uwazi na hali ya kuaminiana, ambavyo ni muhimu katika kuokoa maisha.
"Ninatoa wito kwa nchi ambazo zimeweka marufuku ya usafiri au kufunga mipaka kufikiria upya. Hatua hizi hufanya mwitikio kuwa mgumu zaidi, na zinakatisha tamaa uwazi na hali ya kuaminiana ambavyo huokoa maisha," Tedros amesema.
Licha ya ukosefu wa chanjo zilizoidhinishwa na dawa maalum, mkuu huyo wa WHO amesema wagonjwa bado wanaweza kupona kama watapata huduma ya matibabu kwa wakati unaofaa na iliyo bora.
Tedros amesema ziara yake katika mji huo wa Bunia pia imelenga kushirikiana moja kwa moja na jamii zilizoathiriwa katika mlipuko huo, ambapo visa zaidi ya 1000 vinavyoshukiwa vimeripotiwa.
Uganda pia imeripoti visa tisa vilivyothibitishwa baada ya kubaini maambukizi mawili mapya katika mji mkuu, Kampala, wizara ya afya ya Uganda ilisema Ijumaa.
Waziri wa Afya wa DRC Roger Kamba amesema nchi hiyo inalenga, "katika hali bora zaidi," kudhibiti na kukomesha mlipuko huo ndani ya "miezi minne hadi sita," kulingana na uzoefu wake katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko na sababu inayojulikana ya ugonjwa wa virusi vya Ebola.
Amesema kipaumbele cha haraka ni kudhibiti virusi ndani ya majimbo matatu yaliyoathiriwa -- Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini -- na kuzuia kuenea zaidi.
Kamba pia amesisitiza uwezo ulioimarishwa wa upimaji wa maabara wa nchi hiyo, huku kukiwa hakuna sampuli zilizobaki. Sampuli takriban 900 zimeshapimwa, ambapo takriban 260 zilikutwa na virusi, amesema, huku akiongeza kuwa nchi hiyo sasa ina uwezo wa kushughulikia sampuli zote zinazoingia, hata kama upimaji wa kila siku utaongezeka hadi sampuli 200 au 300.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus akiwasili Bunia, mji mkuu wa Jimbo la Ituri katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mei 30, 2026. (Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



