Wanaharakati wa Kenya walalamikia karantini ya wafanyakazi wa msaada wa Marekani katika kituo cha Ebola kinachozozaniwa

(CRI Online) Julai 23, 2026

Wanaharakati na makundi ya wanasheria wa Kenya wameelezea wasiwasi wao Jumatano baada ya wafanyakazi saba wa msaada wa Marekani kuwekwa karantini ya lazima ya Ebola ya siku 21, kwenye kitengo cha karantini kinachofadhiliwa na Marekani katika Kambi ya Kikosi cha Anga ya Laikipia, Kaunti ya Laikipia, Kenya.

Kituo hicho kilianzishwa kufuatia sera ya Marekani inayotaka raia walio katika hatari ya kuambukizwa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuwekwa karantini katika nchi ya tatu kabla ya kurudi Marekani. Hatua hiyo inakinzana na amri ya awali ya Mahakama Kuu ya Kenya ya kusimamisha kuanzishwa kwa kituo hicho cha karantini ya Ebola kinachoungwa mkono na Marekani nchini humo.

Taasisi ya Katiba, ambalo ni shirika la kiraia la Kenya, awali iliwasilisha kesi ya kutaka kuzuia serikali ya Kenya kuruhusu au kuanzisha vituo vyovyote vya matibabu au karantini ya Ebola vinavyohusiana na nchi za kigeni nchini Kenya. Mahakama Kuu ya Kenya imepanga kusikiliza malalamiko hayo leo Alhamisi, yanayopinga uanzishwaji wa kituo hicho.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha