Lugha Nyingine
Polisi nchini Afrika Kusini wakamata wahamiaji zaidi ya 12,000 wasio na vibali
Polisi wa Afrika Kusini wamesema zaidi ya wahamiaji 12,000 wasio na vibali wamekamatwa kote nchini humo katika wiki tatu zilizopita wakati huu ambapo mamlaka zimeimarisha operesheni za pamoja za kupambana na uhamiaji haramu na uhalifu mkubwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Alhamisi na Idara ya Polisi nchini Afrika Kusini, operesheni hiyo ilitekelezwa kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani, Vikosi vya Ulinzi na vyombo vingine vya kutekeleza sheria.
"Juhudi hizi ni sehemu ya mkakati mpana zaidi wa kuimarisha usalama wa mipaka, kusimamia utekelezaji wa sheria za uhamiaji, na kuhakikisha jamii salama zaidi kwa wote wanaoishi Afrika Kusini." Taarifa hiyo imeeleza.
Imeongeza kuwa operesheni hizo pia zinalenga uhalifu mkubwa, ikiwa ni pamoja na biashara haramu ya dawa za kulevya, umiliki haramu wa silaha, mauaji, ubakaji, wizi, uchimbaji haramu wa madini, uporaji dhidi ya magari ya kusafirisha pesa na shughuli za uhalifu wa kupangwa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



