Iran yasema kutumiana ujumbe na Marekani kunaendelea kupitia wapatanishi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 27, 2026

TEHRAN - Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, amesema Marekani inatumiana ujumbe mbalimbali na Iran kupitia wapatanishi, ikiwemo Pakistan na Qatar, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Iran, zikirejelea kauli zake alizozitoa kwenye mahojiano na shirika la utangazaji la Austria, ORF.

Vyombo vya habari vya Iran vimeripoti Jumapili kuwa, Baghaei amesisitiza kwenye mahojiano hayo kwamba ili mazungumzo yoyote yafanyike, "msingi unaofaa" lazima uwe tayari, akibainisha kuwa Marekani imeharibu msingi wa namna hiyo.

Ameishutumu Washington kwa kukiuka "vifungu vyake vyote" kwa vitendo chini ya nyaraka ya makubaliano (MoU) kati ya Iran na Marekani.

Msemaji huyo amesema kipaumbele cha sasa cha Iran "ni kutetea mamlaka huru ya nchi na ukamilifu wa ardhi ya taifa na kulinda watu wake dhidi ya uhalifu wa kivita ambao unafanywa na Marekani."

Chini ya MoU hiyo iliyosainiwa Juni 18, Marekani na Iran zilikuwa zimepangwa kufanya mazungumzo ndani ya kipindi cha siku 60 ili kufikia makubaliano ya mwisho, lakini hatma ya mazungumzo hayo haina uhakika kufuatia kuanza upya kwa mapigano kati ya pande hizo mbili katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha