Lugha Nyingine
Vikosi vya Marekani vyazuia "shambulio la kushtukiza" la Iran dhidi ya vikosi vya Marekani katika Mashariki ya Kati
WASHINGTON - Jeshi la Marekani limesema kwamba limezuia makombora kadhaa ya balistiki jana Jumanne yaliyorushwa kutoka Iran, kile lilichoeleza kuwa ni jaribio la "shambulio la kushtukiza" dhidi ya vikosi vya Marekani katika Mashariki ya Kati.
"Saa 11:45 jioni ET leo (jana Jumanne), vikosi vya Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu vilirusha makombora kadhaa ya balistiki kutoka Iran katika jaribio la shambulio la kushtukiza dhidi ya vikosi vya Marekani vilivyoko Mashariki ya Kati," Kamandi ya Kati ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) imeandika kwenye mtandao wa kijamii wa X.
"Makombora yote ya Iran yamezuiliwa kwa mafanikio," imesema, ikiongeza "Vikosi vya Marekani vinabaki macho na katika hali ya juu ya utayari."
Kwa mujibu wa ripoti ya CNN, ikimrejelea afisa wa Marekani, Iran imerusha si zaidi ya makombora manne ya balistiki.
Hakukuwa na kauli ya haraka kutoka Tehran juu ya madai hayo ya Marekani.
Mapema siku hiyo ya Jumanne, CENTCOM ilisema jeshi la Marekani lilikuwa limebadilisha mielekeo ya meli 18 za kibiashara zinazopitia Mlango-Bahari wa Hormuz, kuharibu uwezo wa meli mbili na kupanda ndani ya nyingine mbili ili kutekeleza kile ilichokielezea kuwa ni kizuizi cha majini kwa bandari zote za Iran.
CENTCOM pia ilisema katika ujumbe tofauti kwamba meli zaidi ya 20 za kivita za Kikosi cha Majini cha Jeshi la Marekani zinafanya kazi kote Mashariki ya Kati katika kuunga mkono operesheni za kijeshi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



