Lugha Nyingine
Washindi watunukiwa kwa fainali za Afrika za mashindano ya uvumbuzi yanayoungwa mkono na China

Shaukat Abdulrazak, katibu mkuu katika Idara ya Sayansi, Utafiti na Ubunifu ya Kenya, akihutubia hafla ya utoaji tuzo za Fainali za Kanda ya Afrika za Mashindano ya Kimataifa ya Uvumbuzi ya Wanafunzi wa Vyuo vya China 2026 jijini Nairobi, Kenya, Julai 27, 2026. (Xinhua/Yang Guang)
NAIROBI - Timu ishirini zilizoingia Fainali za Kanda ya Afrika za Mashindano ya Kimataifa ya Uvumbuzi ya Wanafunzi wa Vyuo vya China 2026 zimetunukiwa medali za dhahabu na fedha kwenye hafla iliyofanyika Jumatatu wiki hii jijini Nairobi, mji mkuu wa Kenya.
Maafisa waandamizi wa serikali, wanadiplomasia, watendaji wa tasnia, na wahadhiri wa vyuo vikuu walihudhuria hafla hiyo ili kuwapongeza wanafunzi wa vyuo vikuu vya Afrika walio nyuma ya uvumbuzi mpya wa kisasa wenye uwezo wa kubadilisha maisha.
Mashindano hayo ya uvumbuzi ya mwaka huu ambayo yako katika toleo lake la pili, yamevutia washiriki 600 kutoka vyuo vikuu 92 vya Afrika, ambao waliwasilisha miradi 207 inayohusu nyanja mbalimbali, zikiwemo za afya na kilimo.
Baada ya tathimini ya kina, miradi 20 iliorodheshwa kwa ajili ya fainali, huku timu 15 zikitunukiwa medali za fedha, wakati huohuo timu tano zilizoshinda medali za dhahabu zitasafiri kwenda China kwa ajili ya fainali za kimataifa baadaye mwaka huu.
Shaukat Abdulrazak, katibu mkuu katika Idara ya Sayansi, Utafiti na Uvumbuzi ya Kenya, ameyapongeza mashindano hayo kwa kuibua vipaji na ubunifu wa vijana wa Afrika ili kukuza ukuaji unaowanufaisha wote.
Feng Shuyi, makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Nanjing, China amesema, "Lengo letu ni kufanya mashindano haya yawe ya maana zaidi kwa vyuo vikuu vya Afrika na kuhimiza vyema ukuaji na matarajio ya wavumbuzi vijana, kuhakikisha kila timu inapata vyote uzoefu wa thamani na hamasa ya kudumu."
Henry Rotich, mkurugenzi wa vipimo na upimaji katika Ofisi ya Viwango ya Kenya na mjumbe wa jopo la majaji, amesema uvumbuzi ulioonyeshwa na vijana wa Afrika umekidhi viwango vya kimataifa na, mara tu utakapofanyikishwa kibiashara, unaweza kulifanya bara hilo kupiga hatua kubwa hadi katika zama mpya ya viwanda.

Feng Shuyi, makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Nanjing,China akihutubia hafla ya utoaji tuzo za Fainali za Kanda ya Afrika za Mashindano ya Kimataifa ya Uvumbuzi ya Wanafunzi wa Vyuo vya China 2026 jijini Nairobi, Kenya, Julai 27, 2026. (Xinhua/Yang Guang)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



