Mawaziri watatu wa Uganda waapishwa baada ya mzozo wa uraia

(CRI Online) Agosti 12, 2026

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amemuapisha Adonia Ayebare, kuwa waziri mpya wa mambo ya nje wa nchi hiyo jana Jumanne baada ya kuukana uraia wake wa Marekani.

Hafla hiyo ya kuapishwa Ayebare na mawaziri wengine wawili ilifanyika katika Ikulu ya Entebbe, umbali wa kilomita takriban 40 kusini mwa Kampala.

Ayebare, ambaye awali aliwahi kuwa mjumbe wa kudumu wa Uganda katika Umoja wa Mataifa, amechukua nafasi ya Jeje Odongo. Uapisho wake awali ulicheleweshwa kutokana na masuala yanayohusiana na uraia wake pacha.

Museveni amesema kifungu cha kuruhusu uraia pacha kilianzishwa kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za kihistoria, lakini maafisa wa umma lazima waonyeshe utiifu kwa upande mmoja pekee.

Museveni pia alimwapisha Shartsi Kutesa Musherure kuwa waziri wa nchi wa fedha, mipango na maendeleo ya uchumi anayeshughulika na huduma ndogo za fedha, na Juma Witonze Kisekka kuwa waziri wa nchi anayehusika na mambo ya ndani.

Vile vile kuapishwa kwa Musherure awali kulicheleweshwa kutokana na maswali kuhusu uraia wake pacha.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha