Lugha Nyingine
Ushirikiano wa huduma ya afya wa China-Tanzania waleta utambuzi magonjwa kwa kutumia AI kwa wagonjwa

Picha hii iliyopigwa Mei 28, 2026 ikionyesha Yuan Gang, mtaalamu wa mionzi katika kundi la 35 la timu ya matibabu ya China visiwani Zanzibar, akijadili picha za MRI na madaktari wenyeji kwenye Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar, Tanzania. (kundi la 35 la timu ya matibabu ya China visiwani Zanzibar/kupitia Xinhua)
DAR ES SALAAM – Ndani ya chumba cha mionzi katika Hospitali ya Mkoa ya Lumumba visiwani Zanzibar, Tanzania mabadiliko ya kimyakimya ya teknolojia yanabadilisha namna madaktari wanavyobaini magonjwa, kufanya maamuzi, na kuokoa maisha.
Katika kisiwa hicho, mifumo ya akili mnemba (AI) inasaidia madaktari kuchambua picha za kimatibabu, huku mashauriano kwa umbali yakiunganisha madaktari wenyeji na wataalamu walioko maelfu ya kilomita mbali.
Anayeunganisha umbali huu ni Yuan Gang, mtaalamu wa mionzi katika kundi la 35 la timu ya matibabu ya China visiwani Zanzibar, ambaye huchanganya upigaji picha hapo papo, uchambuzi kwa kutumia AI unaotegemea teknolojia ya wingu, na mashauriano ya wataalamu kwa wakati halisi.
Kwa miaka mingi, mfumo wa afya wa Zanzibar umekuwa ukikabiliwa na changamoto katika kubaini magonjwa sugu, hasa kutokana na wataalamu wachache wa upigaji picha, mzigo mkubwa wa kazi, na ukosefu wa vifaa vya hali ya juu vya kubaini magonjwa, anasema daktari mwenyeji Haitham Hamudu.
Haitham amesema, uchambuzi wa picha, ambao mara nyingi huelezewa kuwa ni "macho" ya tiba za kisasa, umekuwa ukitatizwa hasa na utaalamu mdogo, mzigo mkubwa wa kazi, na ukosefu wa vifaa vya hali ya juu.
Kwa kuunganisha mfumo wa upigaji picha wa hospitali hiyo na Hospitali ya Kwanza ya Umma ya Lianyungang katika Mkoa wa Jiangsu mashariki mwa China, ameanzisha mbinu ya utambuzi magonjwa yenye hatua tatu, ambayo inajumuisha vipimo vya awali vinavyofanywa na madaktari wenyeji, ubainishaji na uainishaji unaosaidiwa na AI, na udhibiti wa ubora kupitia mapitio ya wataalamu Wachina.
Mfumo huo mseto unawawezesha madaktari visiwani Zanzibar kufikia usahihi na viwango vya hospitali za kiwango cha juu za China bila kuhitaji wagonjwa kuondoka kisiwani humo.
"Teknolojia inatuwezesha kushinda mapengo ya umbali na rasilimali," Yuan amesema. "Si kuhusu tu kutatua tatizo la mgonjwa mmoja, bali ni kuhusu kujenga mfumo unaoboresha huduma kwa wagonjwa wengi."
Zaidi ya kushughulika na magonjwa ya mtu mmoja mmoja, Yuan ameanzisha zana za upigaji picha zinazowezeshwa na AI ili kuboresha usahihi wa kupima na kubaini magonjwa visiwani Zanzibar.
Vile vile, upigaji picha za mapafu unaosaidiwa na AI unaboresha utambuzi wa mapema wa vinundu vya mapafu ambavyo mara nyingi hupuuzwa katika matokeo ya vipimo vya kawaida.
Zaidi ya upimaji na ubainishaji magonjwa, Yuan anasaidia madaktari wenyeji kutumia zana za AI, mifumo sanifu ya kuripoti, na mbinu za upimaji na ubainishaji magonjwa zilizopangiliwa vema kupitia mafunzo ya vitendo na ufundishaji kulingana na uhalisia wa mgonjwa, kuboresha usahihi wa kubaini magonjwa wakati huohuo ikiimarisha uwezo wa wenyeji.
“Mpango wa upigaji picha kwa AI ni sehemu ya ushirikiano mpana zaidi wa huduma ya afya ya kidijitali kati ya China na Zanzibar ya Tanzania,” Yuan amesema.

Picha hii iliyopigwa Oktoba 8, 2025 ikimuonyesha Yuan Gang, mtaalamu wa mionzi katika kundi la 35 la timu ya matibabu ya China visiwani Zanzibar, akizungumza na mkazi mwenyeji kwenye shughuli ya kutoa huduma ya afya kwa jamii, Zanzibar, Tanzania. (kundi la 35 la timu ya matibabu ya China visiwani Zanzibar/kupitia Xinhua)

Picha hii iliyopigwa Oktoba 8, 2025 ikimuonyesha Yuan Gang, mtaalamu wa mionzi katika kundi la 35 la timu ya matibabu ya China visiwani Zanzibar, akimfanyia kipimo cha ultrasound mgonjwa ndani ya kituo cha afya kwenye shughuli ya kutoa huduma ya afya kwa jamii, Zanzibar, Tanzania. (kundi la 35 la timu ya matibabu ya China visiwani Zanzibar/kupitia Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



