Idadi ya vifo kutokana na ajali ya kupinduka kwa boti nchini Zimbabwe yafikia 84

(CRI Online) Agosti 17, 2026

Jeshi la Polisi nchini Zimbabwe limesema, idadi ya watu waliofariki kutokana na ajali ya kupinduka kwa boti nchini Zimbabwe imefikia 84 kufuatia kuopolewa kwa miili minne jana Jumapili alasiri.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Jumapili na polisi, juhudi za uokoaji bado zinaendelea ili kuwapata waathiriwa ambao bado wameorodheshwa kuwa hawajulikani walipo.

Baadhi ya miili iliyopatikana mapema wiki iliyopita imeruhusiwa kuchukuliwa kwa ajili ya mazishi ndani ya eneo la Ziwa Kariba na maeneo mengine mbalimbali, kwa mujibu wa mamlaka husika.

Boti hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka mji wa Kariba kuelekea Kambi ya Uvuvi ya Chalala nchini humo wakati ajali hiyo ilipotokea kwenye Ziwa Kariba Jumanne jioni, Agosti 11 wiki iliyopita. Mamlaka zimesema watu 77 wameshaokolewa hadi sasa.

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa siku iliyofuata ya Jumatano aliitangaza ajali hiyo kuwa ni janga la taifa, na kuagiza mamlaka husika kutoa msaada kamili kwa familia za waliofariki, ikiwemo uungaji mkono wa kimatibabu, kisaikolojia na mazishi.

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha