Mlipuko wa Ebola nchini DRC wawa uliosababisha vifo vingi zaidi katika historia ya nchi hiyo, idadi ya vifo yazidi 2,300

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Agosti 17, 2026

KINSHASA - Mlipuko wa Ebola unaoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) umekuwa uliosababisha vifo vya watu wengi zaidi katika historia ya nchi hiyo, kufuatia vifo zaidi ya 2,300 kuripotiwa, kwa mujibu wa takwimu rasmi za hivi punde zaidi zilizotolewa jana Jumapili.

Ripoti ya hali iliyotolewa Jumapili na mamlaka za afya za nchi hiyo imerekodi maambukizi 4,945 yaliyothibitishwa, vikiwemo vifo 2,325, tangu mlipuko huo uanze, hali ambayo imeweka kiwango cha vifo katika asilimia 47.0.

Idadi hiyo ya vifo ya hivi punde zaidi imezidi ile ya mlipuko wa Ebola wa 2018-2020 mashariki mwa DRC, ikilifanya janga hilo la sasa kuwa mlipuko wa Ebola uliosababisha vifo vya watu wengi zaidi kuwahi kurekodiwa nchini humo.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mlipuko wa Ebola wa 2018-2020 mashariki mwa DRC ulirekodi maambukizi 3,481, vikiwemo vifo 2,299.

Mlipuko huo wa sasa, ambao ni wa 17 wa Ebola nchini DRC tangu virusi hivyo kugunduliwa kwa mara ya kwanza nchini humo mwaka 1976, ulitangazwa rasmi Mei 15 mwaka huu na umesababishwa na virusi vya Ebola vya spishi ya Bundibugyo.

Mlipuko huo umeathiri kanda 55 za kiafya katika majimbo sita -- Ituri, Kivu Kaskazini, Haut-Uele, Tshopo, Kivu Kusini na Bas-Uele.

WHO imeonya kwamba mlipuko huo wa sasa wa Ebola nchini DRC unaweza kuwa mbaya zaidi kuwahi kurekodiwa.

"Mlipuko huo kwa ukubwa wake tayari ni mlipuko wa pili wa Ebola kuwahi kurekodiwa, na linasonga kwa kasi zaidi kuliko mlipuko wowote wa Ebola uliopita. Kwa kasi yake ya sasa, uko njiani kuupita mlipuko wa Ebola wa Afrika Magharibi wa 2014 hadi 2016," Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus aliuambia mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva Jumatano wiki iliyopita.

Janga la Ebola la Afrika Magharibi la mwaka 2014-2016, ambalo ni mlipuko mkubwa zaidi wa Ebola kuwahi kurekodiwa, liliathiri watu zaidi ya 28,600.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha