Lugha Nyingine
Rais wa Afrika Kusini aihimiza SADC kukabiliana na vyanzo vya uhamiaji
DURBAN, Afrika Kusini - Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametoa wito kwa nchi za Kusini mwa Afrika kukabiliana na vyanzo vinavyosababisha uhamiaji wakati huohuo zikifanya kazi kuelekea uhuru mkubwa zaidi wa watu kuhama na kusafiri katika eneo hilo chini ya Dira ya 2050 ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Akizungumza siku ya Ijumaa katika Chuo Kikuu cha KwaZulu-Natal kwenye mji wa pwani wa Durban wa Afrika Kusini kabla ya Mkutano wa 46 wa Viongozi wa SADC, Ramaphosa amesema mafungamano ya kikanda yanapaswa hatimaye kuruhusu watu kuhama kwa uhuru kulingana na kanuni, itifaki na sheria zilizowekwa, wakati huohuo yakihakikisha kwamba uhamiaji unachochewa na chaguo badala ya hali ya kutokuwa na matumaini.
Ramaphosa pia amelaani ubaguzi na unyanyasaji dhidi ya raia wa kigeni wakati ambapo mivutano juu ya uhamiaji nchini Afrika Kusini inaongezeka.
"Vitendo vya uhalifu vya wachache ndani ya jamii zetu ni kukiuka mshikamano ambao ndio msingi wa kuanzishwa kwa jumuiya hii. Hatuwezi kuhubiri mafungamano katika mikutano na kutekeleza ubaguzi katika mitaa yetu," ameongeza.
Mwezi Juni, Ramaphosa alitangaza mpango wa usimamizi wa uhamiaji wenye vipengele vitano. Mpango huo unajumuisha utekelezaji mkali zaidi wa sheria za uhamiaji na kazi, usalama ulioimarishwa wa mipaka, maboresho ya mifumo ya usimamizi wa uhamiaji, mapitio ya mapengo katika sheria na sera, na ushirikiano imara zaidi na nchi nyingine za Afrika.
Tangu wakati huo serikali imeongeza operesheni za kuwafukuza nchini na kuwarejesha watu katika nchi zao. Kwa mujibu wa taarifa mpya kutoka kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Mipaka ya nchi hiyo wiki hii, watu karibu 90,000 walikuwa wameshaondoka Afrika Kusini katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
Mkutano wa 46 wa Viongozi wa SADC umepangwa kufanyika leo Jumatatu Agosti 17 jijini Durban chini ya mada "Maendeleo ya viwanda yaliyo himilivu, endelevu na jumuishi kupitia maendeleo ya miundombinu, mabadiliko ya kilimo na madini muhimu katika kujenga dunia ya haki."
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



