Lugha Nyingine
Matumizi ya RMB yapanuka barani Afrika kutokana na kukua kwa muunganisho wa kifedha na biashara

Wageni wakisherehekea uzinduzi wa huduma ya malipo ya moja kwa moja kwa RMB ya Benki ya Stanbic Tanzania jijini Dar es Salaam, Tanzania, Agosti 12, 2026. (Xinhua/Nurdin Pallangyo)
NAIROBI - Sarafu ya China, renminbi (RMB), inabeba jukumu kubwa zaidi barani Afrika wakati huu ambapo biashara na Afrika ikistawi.
Kuanzia uzinduzi wa huduma za malipo ya moja kwa moja kwa RMB nchini Tanzania hadi muunganisho uliopanuliwa na Mfumo wa Malipo wa Kati ya Benki wa Kuvuka Mpaka (the Cross-Border Interbank Payment System, CIPS) nchini Kenya na Namibia, vilevile kuanzishwa kwa mipangilio ya malipo kwa RMB kwa Afrika, maendeleo hayo ya hivi karibuni yanaonyesha jukumu linalozidi kuongezeka la sarafu ya China katika miamala ya kuvuka-mipaka.
Kadri biashara ya China na Afrika inavyoendelea kupanuka, RMB inatumika si tu kwa malipo ya biashara, bali inatumika zaidi katika malipo ya moja kwa moja na mipangilio ya malipo na, hivi karibuni, kwa mambo ya kifedha. Upanuzi huu unaechochewa na mahitaji yanayozidi kuongezeka kutoka kwenye biashara na uwekezaji kati ya China na Afrika, huku miundombinu ya kifedha iliyoboreshwa ikifanya miamala ya RMB ya kuvuka-mipaka ipatikane kirahisi zaidi.
Matumizi ya kimataifa ya sarafu yanahusiana kwa karibu na mahitaji yanayotokana na biashara na uwekezaji. Kuendelea kwa kina kwa uhusiano wa kiuchumi kati ya China na Afrika kunatoa uungaji mkono imara zaidi kwa matumizi mapana ya RMB katika miamala ya kuvuka-mipaka.
Mwezi Agosti, Benki ya Stanbic Tanzania ilizindua huduma ya malipo ya moja kwa moja kwa RMB, ikiruhusu kampuni za Tanzania zinazofanya biashara na China kufanya na kupokea malipo moja kwa moja katika RMB.
“Malipo ya moja kwa moja kwa RMB yanaweza kupunguza ubadilishaji wa sarafu usio wa lazima na unazipa kampuni chaguo la ziada la malipo,” Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara wa Tanzania Dennis Londo alisema.
Nchini Zambia, RMB pia imekuwa ikitumika kwa malipo ya kodi ya madini. Benki kuu ya nchi hiyo ilianza kukubali malipo ya RMB kwa kodi ya madini mwezi Oktoba 2025.
Kwa Zambia, ambako mauzo ya nje ya shaba ni nguzo kuu ya kiuchumi na China ni mshirika wake muhimu wa biashara, njia hiyo ya malipo kwa RMB huzipa kampuni na serikali chaguo jingine la kusimamia mahitaji ya kubadilisha fedha za kigeni.
Nchi zingine nyingi za Afrika zikiwemo Kenya, Afrika Kusini, Namibia, Mauritius na Misri nazo kwa namna moja au nyingine zimeanzisha utaratibu wa kuwa na huduma mbalimbali zinazohusisha RMB.
Kwa mujibu wa Ripoti ya 2025 ya Kuifanya RMB Kuwa ya Kimataifa ya Benki Kuu ya China, ujumla wa kupokea na kulipa kwa RMB kati ya China na Afrika ulifikia yuan bilioni 155.33 (dola bilioni 23.14) mwaka 2024, ongezeko la asilimia 28.1 kutoka mwaka uliotangulia wa 2023. Upokeaji na ulipaji wa RMB unaohusiana na biashara ya bidhaa ulifikia yuan bilioni 56.37 (dola bilioni 8.4), ongezeko la asilimia 35.9.
Ripoti hiyo inaonesha kuwa, kuanzia 2020 hadi 2024, malipo kwa RMB ya kuvuka-mipaka kati ya China na Afrika yaliongezeka maradufu, kutoka yuan bilioni 80.02 (dola bilioni 11.92) hadi yuan bilioni 155.33 (dola bilioni 23.14), ikiwakilisha kiwango cha wastani cha ukuaji kwa mwaka cha asilimia 18.1.
Huang Meibo, mkuu wa Taasisi kwa ajili ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Biashara na Uchumi wa Kimataifa cha Shanghai, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba miundombinu bora ya malipo inafanya miamala ya RMB ya kuvuka-mipaka kuwa rahisi zaidi katika masoko ya Afrika.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



