Lugha Nyingine
ChinaVumbuzi | China yatambua kazi 11 mpya kutokana na viwanda vya kazi za aina mpya vinavyojitokeza

Mfanyakazi akiifundisha roboti ya umbo la binadamu kuchanganua na kupanga tyubu za uzi kwenye kituo cha kuzifanyia mafunzo roboti za umbo la binadamu katika Mji wa Cixi mkoani Zhejiang, mashariki mwa China, Septemba 3, 2026.(Xinhua/Xu Yu)
BEIJING - China imetambua rasmi kazi 11 za aina mpya na fani mpya 23 chini ya kazi zilizopo sasa, hali ambayo imeonesha mabadiliko ya mahitaji ya kazi kutokana na maendeleo ya teknolojia, uboreshaji wa viwanda na mahitaji ya matumizi.
Kazi hizo za aina mpya zilizotangazwa jana Jumatano na Wizara ya Rasilimali Watu na Uhakikisho wa Kijamii ya China na idara nyingine za serikali, zinahusisha mafundi wa uhandisi wa usimamizi wa meli katika maeneo ya pwani, mafundi wa roboti za AI za maumbo ya binadamu na wachambuzi wa data za michezo.
Mamlaka hizo pia zimezifanyia marekebisho taarifa kuhusu kazi au fani sita zilizopo sasa, ikiwa ni pamoja na madalali wa mazao ya kilimo.
Kutambua kazi na fani hizo mpya kutasaidia kuhimiza utoaji nafasi za ajira na ujasiriamali, kuwapa wafanyakazi njia mbalimbali zaidi za kujipatia kazi, na kulinganisha vizuri zaidi utoaji wa vipaji na mahitaji ya nafasi za ajira.
Tano kati ya kazi hizo mpya zilizotambuliwa zimeainishwa kuwa ni kazi za kidijitali na tatu kuwa ni kazi za kijani, na kufanya jumla husika nchini China kufikia 113 na 142.
Ofisa mmoja wa wizara hiyo amesema China inakadiriwa kukabiliwa na upungufu mkubwa wa wafanyakazi wenye ujuzi wa kidijitali ndani ya muda fulani, na ameongeza kuwa kutambua kazi hizo aina mpya kutachochea kazi ya utoaji mafunzo na kuleta hali nzuri ya baadaye ya utoaji wa nafasi nyingi za ajira.
Amesema, kuongezwa kwa kazi hizo mpya pia kunadhihirisha upanuzi unaoendelea wa huduma za kiteknolojia na kiujuzi.
Amesema baadhi ya kazi hizo za aina mpya zinahusiana zaidi na maendeleo ya biashara na uboreshaji wa viwanda, ikiwa ni pamoja na wapangaji wa maendeleo endelevu ya kampuni, wakaguzi wa kazi ya kuondoa vitu vya vizuizi kwenye viwanja vya ndege, na waanzilishi wa programu za kompyuta zinazotegemea AI. Kazi nyingine ni zinazoweza kukidhi moja kwa moja zaidi mahitaji ya watu juu ya huduma zenye ubora wa juu zaidi, ikiwa ni pamoja na mafundi wa kutengeneza uvumba, wafanyakazi wa kuunganisha sehemu za samani na kuzikamilisha kwa teknolojia janja, na wafanyakazi wa kuandaa maua freshi.
Tokea mwaka 2019, China imetangaza kwa mara nane kazi mpya 121 kwa jumla.
Kati ya kazi hizo mpya, asilimia 60 zinahusiana na kazi za huduma, wakati kazi za kitaaluma na kiufundi na kazi husika za utengenezaji bidhaa kila moja inachukua asilimia 17.
Kwa kuangalia hali ya kazi mbalimbali, asilimia 43 ya kazi hizo mpya ni kazi za huduma za kiteknolojia na kiujuzi, na nyingine asilimia 34 ni kazi za utengenezaji bidhaa kwa teknolojia ya kisasa.
Katika kipindi cha Mpango wa 15 wa Miaka Mitano (2026-2030), China inalenga kutafuta namna ya kutoa nafasi mpya za ajira katika wakati wa kuendeleza uchumi wa kidijitali, uchumi wa kijani na uchumi wa kazi zinazohusu huduma za wazee.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



