China inaweka mazingira mazuri ya uzazi kwa kuboresha huduma

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 15, 2026

China itachukua hatua zaidi kusaidia malezi ya watoto, ikiwa ni pamoja na kufanya huduma za malezi ya watoto kupatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu, ili kujenga jamii yenye mazingira mazuri kwa uzazi, na kuongeza kiwango cha kuzaliwa kwa watoto.

Mkuu wa Kamati ya Kitaifa ya Afya ya China (NHC), Bw. Lei Haichao, amesema juhudi endelevu zitafanywa ili kuhimiza maendeleo jumuishi ya huduma katika shule za awali na vituo vya malezi ya watoto, na kusaidia maeneo ya wakazi pamoja na idara za waajiri kuanzisha vituo vya kutunza watoto.

China pia itafanya juhudi za kuongeza upatikanaji wa huduma za kutunza watoto wadogo ili kupunguza mzigo wa gharama kwa familia ya kuwa na watoto, kuwalea na kugharamia elimu ya watoto. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu, idara nyingine 1,000 za matibabu na afya katika ngazi ya eneo la wakazi, zitaweza kutoa huduma za matibabu kwa watoto.

China imeunda mfumo kamili wa kusaidia uzazi unaohusisha hatua za kabla ya ujauzito, kipindi cha ujauzito, kujifungua na malezi ya watoto, unaohusisha posho ya uzazi, ruzuku za malezi ya watoto, urejeshaji wa gharama za bima ya afya na huduma za malezi ya watoto kwa gharama nafuu, ili kupunguza mzigo wa kifedha kwa familia zenye watoto.

Bw. Lei pia amesema jumla ya kliniki 12,562 za huduma za awali za ujauzito zimeanzishwa, zikiwepo kwenye karibu wilaya zote. Wanawake wajawazito wanaweza kwenda kliniki hizi katika hatua za awali za ujauzito ili kupata ushauri na huduma nyinginezo, na kama kuna hatari ya kuharibika kwa mimba, kliniki hizo zinaweza kuwasaidia kutathmini hatari hiyo na kuchukua hatua za kinga.

Mwaka 2025, viwango vya vifo vya akina mama na watoto wachanga nchini China vilishuka hadi kufikia 13.4 kati ya uzazi hai 100,000, na 3.8 kwa kila uzazi hai 1,000 mtawalia. Hali hii inaifanya China iwe kati ya nchi zinazoongoza katika takwimu hizi kati ya nchi zenye mapato ya kati ya juu na ya juu, pamoja na nchi zenye idadi ya watu inayozidi milioni 100.

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha