Lugha Nyingine
CIIE yafungwa ikiweka rekodi katika kuisainiwa kwa makubaliano ya biashara zilizooneshwa kwa mara ya kwanza duniani

Picha hii iliyopigwa tarehe 10 Novemba 2026 ikionesha uwanja wa kusini wa Kituo cha Kitaifa cha Mikutano na Maonesho (Shanghai), eneo kuu la Maonesho ya 9 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa Nje ya China (CIIE), mjini Shanghai, mashariki mwa China. (Xinhua/Wang Xiang)
SHANGHAI - Maonesho ya 9 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa Nje ya China (CIIE) yamefungwa mjini Shanghai jana Jumanne, ofisa katika Ofisi ya CIIE Xiao Lu amejulisha kuwa, thamani ya makubaliano yenye nia ya ushirikiano wa muda wa mwaka mmoja yamefikia rekodi ya juu kabisa ya dola bilioni 85.45 za Marekani, ambayo ni ongezeko la asilimia 2.3 ikilinganishwa na maonesho yaliyopita.
Maonesho hayo ya mwaka huu yalivutia kampuni 4,142 kushiriki kwenye maonesho, idadi ambayo imevunja rekodi, na ukubwa wa eneo lake la maonesho ya kibiashara pia umevunja rekodi na kufikia mita za mraba 370,000. Kwa mara ya kwanza, idadi ya kampuni zilizoshiriki kwenye maonesho ambazo ziko kwenye orodha ya Kampuni Bora 500 duniani (Fortune Global 500) pamoja na kampuni za kuongoza sekta mbalimbali ilizidi 300.
Maonesho hayo ya siku sita yalionesha bidhaa 485 ambazo zilionekana kwa mara ya kwanza duniani, barani Asia, au nchini China, idadi ambayo imeongezeka kuliko zile 461 za mwaka uliopita na kuweka rekodi mpya.
Kampuni za Marekani kwa mwaka wa nane mfululizo zimechukua eneo kubwa zaidi la maonesho kuliko nchi nyingine na maeneo mengine vilivyoshiriki, zikichukua eneo la mita za mraba zaidi ya 50,000. Na mwaka huu ukubwa wa mabanda ya maonesho bila malipo yaliyoandaliwa kwa nchi zilizoko nyuma zaidi kimaendeleo uliongezeka kwa asilimia 17, hali ambayo iliwezesha ushiriki mpana zaidi kwenye maonesho hayo.
Maonesho hayo yalifanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2018 yakiwa ni maonesho ya kwanza duniani ya ngazi ya kitaifa yanayolenga uagizaji bidhaa, na ni sehemu ya juhudi za China za kupanua uagizaji bidhaa kutoka nje, na pia kutoa jukwaa kwa wafanyabiashara wa kimataifa kuonesha bidhaa zao na kuwasiliana moja kwa moja na wanunuzi wa China.
Katika maonesho ya vivutio vya teknolojia mwaka huu, kampuni ya Marekani inayotengeneza chipu, Qualcomm, ilionesha mashine ya kwanza ya 6G duniani nje ya mazingira ya maabara, na kampuni kubwa ya uhandisi ya Ujerumani, Bosch, ilionesha kwa mara ya kwanza duniani mfumo wa kudhibiti tabianchi nyumbani unaoendeshwa kwa teknolojia ya AI ambao unaweza kuboresha viwango vya joto na matumizi ya nishati.
Maonesho hayo pia yameleta jukwaa la kufanya maonesho kwa ajili ya wavumbuzi wapya. Sehemu ya kulea na kukuza uvumbuzi ya maonesho ya mwaka huu ilihusisha miradi 633 kutoka nchi na maeneo karibu 40, ikiwa ni ongezeko la karibu asilimia 20 ikilinganishwa na maonesho ya mwaka uliopita.

Watu wakiondoka kwenye eneo la Maonesho ya 9 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa Nje ya China (CIIE) mjini Shanghai, mashariki mwa China, tarehe 10 Novemba 2026. (Xinhua/Liu Lingyi)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



