Lugha Nyingine
Russia, Ukraine na Marekani zakamilisha siku ya kwanza ya mazungumzo ya pande tatu; kuendelea tena leo Jumatano

Picha hii ikionesha raundi mpya ya mazungumzo ya pande tatu yanayohusisha Russia, Marekani na Ukraine mjini Abu Dhabi, Falme za Kiarabu, tarehe 10 Novemba 2026. (WAM/kupitia Xinhua)
ABU DHABI - Russia, Ukraine na Marekani zimekamilisha siku ya kwanza ya mazungumzo ya pande tatu mjini Abu Dhabi, mji mkuu wa Falme za Kiarabu, jana Jumanne baada ya masaa karibu manne ya mazungumzo huku mazungumzo hayo yakiwa yamepangwa kuendelea tena leo Jumatano.
Mazungumzo hayo ni ya kwanza ya pande tatu kati ya nchi hizo tatu tangu mwezi Februari.
Ujumbe wa Russia unaongozwa na msaidizi wa rais, Vladimir Medinsky, na unajumuisha Naibu Mawaziri wa Mambo ya Nje, Sergei Ryabkov na Mikhail Galuzin, pamoja na mkuu wa idara ya ujasusi wa kijeshi, Igor Kostyukov, miongoni mwa maafisa wengine.
Wajumbe maalum wa Marekani, Steve Witkoff na Jared Kushner, wanaongoza ujumbe wa Marekani.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Interfax-Ukraine, likimnukuu mshauri wa mawasiliano wa rais wa Ukraine, Dmytro Lytvyn, ujumbe wa Ukraine unajumuisha Rustem Umerov, mkuu wa Idara ya Ujasusi wa Nje ya Ukraine, na Kyrylo Budanov, mkuu wa Ofisi ya Rais, vilevile maafisa wengine.
Katika hotuba ya ufunguzi, Medinsky ameelezea matumaini kwamba mkutano huo utasaidia kusukuma mbele amani kwa manufaa ya watu wa Russia na Ukraine, huku Umerov akisema kuwa raundi hiyo ya sasa ya mazungumzo inalenga kufikia amani ya kudumu.
Kabla ya mazungumzo hayo ya pande tatu, timu ya Ukraine ilikutana na wawakilishi kutoka Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Italia, vilevile maafisa kutoka NATO na Kamisheni ya Ulaya. Mkutano huo pia ulihudhuriwa na wajumbe maalum wa Marekani, Steve Witkoff na Jared Kushner.
Baada ya siku hiyo ya kwanza ya mazungumzo, maafisa wa Ukraine na Marekani wameyaelezea mazungumzo hayo kuwa ya kiujenzi na yenye tija.
Baadaye siku hiyo, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba mazungumzo hayo ya pande tatu yalikuwa "yenye tija na ya kina," huku washiriki wakijadili hatua zinazowezekana za kibinadamu, ikiwemo kuachiliwa kwa wafungwa, jambo alilolielezea kuwa ni la kipaumbele.
Zelensky aliongeza kuwa mazungumzo hayo yataendelea siku ya Jumatano, akisisitiza kuwa lengo kuu ni "kuleta amani karibu zaidi."
Akizungumza baada ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa kundi la G7 jijini Paris, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio aliyaelezea mazungumzo hayo kuwa "yenye tija kubwa," akisema kuwa muundo huo wa pande tatu unapaswa hatimaye kupanuliwa ili kujumuisha washirika wa Ulaya.
Siku ya Jumanne, Jeshi la Anga la Ukraine kilisema kuwa Russia ilirusha droni 162 na kombora moja la balistiki kuelekea Ukraine wakati wa usiku, huku Wizara ya Ulinzi ya Russia ikisema kuwa vikosi vyake vilizuia na kuharibu droni 162 za Ukraine. Madai hayo ya kijeshi hayakuweza kuthibitishwa na vyanzo huru.

Picha hii ikionesha raundi mpya ya mazungumzo ya pande tatu yanayohusisha Russia, Marekani na Ukraine mjini Abu Dhabi, Falme za Kiarabu, tarehe 10 Novemba 2026. (WAM/kupitia Xinhua)

Picha hii iliyopigwa Novemba 3, 2026, ikionesha eneo la makazi wakati umeme ukiwa umekatika mjini Kiev, Ukraine. (Xinhua/Li Dongxu)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



