Tanzania yapokea dozi za chanjo za Sinopham kutoka China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 09, 2021
Tanzania yapokea dozi za chanjo za Sinopham kutoka China

DAR ES SALAAM, Oktoba 8 (Xinhua) - Tanzania Ijumaa hii imepokea dozi 1,065,600 za chanjo ya Sinopharm kutoka China chini ya COVAX, ikiongeza kampeni ya chanjo ya taifa hilo la Afrika Mashariki dhidi ya COVID-19.

 Akizungumza muda mfupi baada ya kupokea chanjo hizo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dorothy Gwajima alitoa shukrani kwa chanjo hizo, akisema msaada huo utasaidia kuharakisha kampeni ya chanjo ya Tanzania iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan mnamo Julai 28.

 COVAX ni mpango wa kimataifa unaolenga kufikia usawa wa chanjo za COVID-19.

 Alisema jumla ya raia 760,962 wamepewa chanjo katika Tanzania Bara huku Zanzibar jumla ya raia 10,800 wamepokea chanjo kufikia Oktoba 7.

Xu Chen, Naibu Balozi katika Ubalozi wa China nchini Tanzania, alisema chanjo zilizotolewa zitasaidia vita vya Tanzania dhidi ya janga hilo.

Alisema serikali ya China na Wizara ya Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania zinashirikiana kwa karibu sana kuwezesha uchangiaji wa shehena mbili za chanjo ambazo zina jumla ya dozi milioni 1.5 za chanjo za COVID-19 kutoka China.

Sherehe za makabidhiano ya chanjo hizo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere katika mji mkuu wa kibiashara Dar es Salaam zilihudhuriwa na maafisa wa ngazi ya juu serikalini na wawakilishi kutoka Umoja wa Mataifa, Shirika la Afya Duniani WHO na Shirika la kuwahudumia Watoto wa Umoja wa Mtaifa UNICEF. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Renato Lu)

Picha