Mwenge wa Olimpiki kwa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing 2022 wawashwa Ugiriki

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 19, 2021
Mwenge wa Olimpiki kwa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing 2022 wawashwa Ugiriki
(Picha zinatoka tovuti ya Shirika la Habari la China Xinhua.)

OLIMPIA YA KALE, Ugiriki - Mwenge wa Olimpiki ambao utawaka wakati wa Michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi itakayofanyika, jijini Beijing, China mwaka 2022 umeanza safari yake baada ya kuwashwa rasmi mahali ya chimbuko la michezo hiyo huko Olimpia ya Kale, Ugiriki Jumatatu wakati wa hafla ya kuwasha mwenge huo.

Mwigizaji Xanthi Georgiou akiigiza uhusika wa Kuhani Mkuu wa zamani wa Ugiriki ametumia kioo mbinuko kuangazia miale ya jua na kuwasha mwenge mbele ya Hekalu la kale la Hera lenye miaka 2,500, ambaye ni mungu wa kike katika hadithi za zamani za Ugiriki.

Rais wa Ugiriki Katerina Sakellaropoulou, Mwenyekiti wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) Thomas Bach, mwakilishi maalum na Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing 2022 Yu Zaiqing walihudhuria hafla hiyo ambayo ilifanyika bila watazamaji chini ya hatua kali za UVIKO-19.

Katika hotuba yake, Bach amesema "Katika dunia yetu hii tete, ambapo utengano, mgawanyiko na hali ya kutokuaminiana vimeongezeka, Michezo ya Olimpiki daima hujenga madaraja na urafiki."

Ameongeza kuwa, "Beijing itakuwa mji wa kwanza katika historia wa kufanya Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Joto (2008) na Majira ya Baridi. Michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi ya Beijing ya Mwaka 2022 itaunganisha watu wa China na dunia, na kutimiza lengo la China la kushirikisha watu milioni 300 katika michezo kwenye theluji na barafu, kubadili michezo ya majira ya baridi daima. Ulimwengu wote utashuhudia shauku hii wakati China itakapokaribisha wanamichezo bora wa michezo ya majira ya baridi."

Kabla ya ibada ya kijadi ya kuwasha moto, Meya wa Olimpia ya Kale Georgios Georgiopoulos na Spyros Capralos, Mwenyekiti wa Kamati ya Olimpiki ya Hellenic na mwanachama wa IOC, pia walihutubia hafla hiyo.

"Tuna hakika kwamba, kama ulivyoonesha katika siku za hivi karibuni, utaandaa Michezo bora ya Olimpiki, kwa kuzingatia uzuri na heshima ya nchi yako, na fahari na maadili ya kamati ya Olimpiki yenyewe," alisema Georgiopoulos.

Yu Zaiqing, ambaye pia ni naibu mwenyekiti wa IOC, aliunga mkono kwa kusema "Mwenge wa Olimpiki umetuletea ujasiri, ukarimu na matumaini wakati wa Janga la UVIKO-19. Imekuwa chanzo cha nguvu katika mapambano yetu dhidi ya janga hilo. Kushirikiana kujenga mustakabali wa pamoja".

Mwenge huo wa Olimpiki utakabidhiwa kwa waandaaji wa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing 2022 Jumanne ya wiki hii kwenye Uwanja wa Panathenaic huko Athens, Ugiriki kabla ya kuwasili China Jumatano ya wiki hii.

Karibu wanariadha 2,900, wanaowakilisha Kamati za Olimpiki za nchi na sehemu 85, wanatarajiwa kushindana katika Michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi ya mwaka 2022. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha