Kuimarishwa kwa vizuizi dhidi ya UVIKO-19 kwazua maandamano, ghasia kote Ulaya katikati ya wimbi jipya la janga (3)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 23, 2021
Kuimarishwa kwa vizuizi dhidi ya UVIKO-19 kwazua maandamano, ghasia kote Ulaya katikati ya wimbi jipya la janga
Picha iliyopigwa Novemba 1, 2021 katika moja ya maduka mjini Amsterdam, Uholanzi ikionesha tangazo la tahadhari dhidi ya UVIKO-19 la kutaka watu kuweka umbali wa mita 1.5 (Xinhua/Sylvia Lederer)

PARIS, Ufaransa - Ili kukabiliana na hatua zilizoimarishwa za kuzuia maambukizi ya UVIKO-19, maandamano yanaendelea kufanyika katika miji mbalimbali barani Ulaya huku kukiwa na ongezeko la visa vya maambukizi ya virusi vya korona na wimbi jipya la janga.

Nchini Ubelgiji na Uholanzi, maandamano hayo yalizidi kuwa ghasia, hali ambayo ilisababisha polisi kutumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha.

Takriban watu 35,000 walikusanyika katikati mwa Brussels, Mji Mkuu wa Ubelgiji siku ya Jumapili kuandamana dhidi ya hatua zilizoimarishwa dhidi ya UVIKO-19 ambazo zilianza kutekelezwa wikendi iliyopita.

Kwa mujibu wa serikali ya Brussels, hatua hizo ni pamoja na matumizi ya lazima ya vyeti vya kutokuwa na maambukizi ya UVIKO-19 (CST) na wajibu wa kuvaa barakoa katika maeneo ambayo CST inahitajika.

Huko Rotterdam, Uholanzi maandamano dhidi ya vizuizi vya UVIKO-19 yalianza jioni ya Ijumaa iliyopita wakati mamia ya waandamanaji walipokusanyika katikati mwa jiji hilo wakirusha fataki na kuchoma moto magari, miongoni mwao angalau gari moja la polisi liliwaka moto.

Maandamano hayo yalizidi kuwa ghasia, na polisi walilazimika kutumia maji ya kuwasha na mabomu ya machozi. Takriban watu 50 walikamatwa na wanne walijeruhiwa na kupelekwa hospitalini kwa matibabu.

Siku ya Jumatatu, Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte alilaani ghasia za siku tatu zilizopita katika miji mbalimbali nchini humo na kuonya kwamba kila linalowezekana litafanywa kuwaadhibu wafanya ghasia.

Maeneo mengi ya Ugiriki, mikahawa na baa yalisalia kufungwa wiki iliyopita katika maandamano dhidi ya vizuizi vipya vya serikali dhidi ya UVIKO-19.

Shirikisho la Panhellenic la Migahawa na Taaluma Zinazohusiana (POESE) lilitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikisema kuwa, hatua hizo zimeathiri sana maelfu ya biashara, huku nyingi kati ya biashara hizo zikikabiliwa na hatari ya kufungwa kwa kudumu, na uungaji mkono wa serikali unahitajika zaidi.

Majira ya baridi yanapowasili katika Ulimwengu wa Kaskazini, Umoja wa Ulaya (EU) unahofia kutokea kwa wimbi jipya la maambukizo ya UVIKO-19.

Kituo cha Ulaya cha Kinga na Udhibiti wa Magonjwa (ECDC) Ijumaa iliyopita kimetangaza makadirio yake ya kiwango cha wasiwasi kuhusu hali ya UVIKO-19 katika Umoja wa Ulaya kuwa 8.3 kati ya 10, au "juu sana". .

Kuvaa barakoa, kunawa mikono na kuingiza hewa ni hatua muhimu zisizo za dawa ambazo lazima ziendelee ili kupambana na UVIKO-19, na "inabakia kuwa muhimu sana kufuata hatua zisizo za dawa," amesema Stefan De Keersmaecker, Msemaji wa Kamati ya Ulaya anayeshughulikia mambo ya Afya, amesema Jumatatu ya wiki hii.

Kwa kuzingatia hali inayozidi kuwa mbaya, Baraza la Uelekezi la Mkakati wa Chanjo la Ufaransa (COSV) siku ya Jumatatu lilipendekeza kwamba chanjo za nyongeza kwa watu wazima wote zinapaswa kuzingatiwa.

Aidha, majimbo mbalimbali ya Ujerumani hivi karibuni yameimarisha hatua zao dhidi ya UKVIO-19. Gernot Marx, Mwenyekiti wa Chama cha Wataalamu wa Kijerumani kwa ajili ya Huduma ya Wagonjwa Mahututi na Tiba ya Dharura (DIVI), amesema katika hafla iliyorushwa moja kwa moja Jumatatu kwamba "hali ya UVIKO-19 (nchini Ujerumani) inatia wasiwasi sana na haidhibitiwi kwa sasa"

Kutokana na hali hiyo ya kuongezeka kwa visa vya UVIKO-19, Shirika la Habarri la AFP, limeripoti kwamba Marekani kupitia Wizara ya Mambo ya Nje imetoa ushauri kwa raia wa Marekani wa kutosafiri katika nchi za Ujerumani na Denmark. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha