Bidhaa za China zapata umaarufu Afrika wakati Ijumaa Nyeusi ya Ununuzi ikikaribia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 25, 2021
Bidhaa za China zapata umaarufu Afrika wakati Ijumaa Nyeusi ya Ununuzi ikikaribia
Mfanyakazi akifanya kazi kwenye ghala la Kampuni ya Biashara ya Mtandaoni ya Jumia mjini Lagos, Nigeria, Septemba 13, 2019. (Xinhua/Guo Juni)

GUANGZHOU/NAIROBI, Bidhaa za China zimeonekana kuongezeka umaarufu kwenye majukwaa ya biashara ya mtandaoni barani Afrika wakati wa msimu wa ununuzi wa Ijumaa Nyeusi ulioanza mapema Mwezi Novemba mwaka huu.

Jumia ni moja ya majukwaa makubwa ya biashara ya mtandaoni barani Afrika linalotumiwa katika nchi 11 za Afrika na idadi ya watumiaji wamefika milioni 7 hadi kufikia Novemba mwaka huu. Jason Cheng, Meneja Mkuu wa Jumia Global, waendeshaji wa jukwaa hilo amesema kuwa zaidi ya wachuuzi 2,000 wa China wamejiunga na jukwaa hilo, ambalo sasa linachukua zaidi ya bidhaa milioni 14 za China.

"Bidhaa za China, hasa vifaa vya simu, nguo na vifaa vya nyumbani, vinanunuliwa zaidi miongoni mwa wanunuzi wa Afrika," Cheng amesema.

Hadi sasa Uuzaji wa bidhaa za China kwenye jukwaa hilo wakati wa msimu wa ununuzi wa Ijumaa Nyeusi umechangia asilimia 18 ya mauzo yote, kiasi ambacho kimeongezeka kutoka asilimia 15 ya mwaka jana kipindi kama hicho.

Katika nchi za Ivory Coast na Ghana, mauzo ya bidhaa za China yalichukua zaidi ya asilimia 45 na asilimia 50 ya jumla ya mauzo yote.

Wafanyabiashara kutoka China wanawavutia wateja wa Afrika kwa punguzo kubwa kwenye jukwaa la mtandaoni wakati wa msimu huo.

Kwa mfano, Kampuni ya TECNO Mobile, chapa maarufu ya simu za mkononi ya China barani Afrika, inatoa punguzo la zaidi ya asilimia 30 kwa baadhi ya miundo ya simu kwenye Jukwaa la Jumia. Aidha, chapa ya mtindo wa mavazi ya China ya SHEIN nayo imetoa punguzo la juu hadi asilimia 75.

Edith Mokeira, mwandishi wa mtandaoni anayeishi Kenya, aliliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba anapenda kununua bidhaa za kielektroniki za China, viatu na nguo kupitia mtandaoni.

Kwa mujibu wa Cheng, Jukwaa la Mtandaoni la Jumia limefikia makubaliano ya kimkataba ya ushirikiano na chapa nyingi maarufu za China kama vile Huawei, Xiaomi, Konka na Xtep.

Meneja wa Kilimall, Lu Xiaoyong mojawapo ya majukwaa makubwa ya mtandaoni ya China katika Afrika Mashariki, amesema jukwaa lake lina zaidi ya wachuuzi 1,000 wa Afrika na limetoa nafasi za ajira 10,000 kwa wenyeji.

Kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa za China kunaashilia kuimarika kwa ushirikiano wa biashara ya mtandaoni kati ya China na Afrika.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Biashara ya China, biashara kati ya China na Afrika iliongezeka kwa asilimia 38.2 na kufikia dola za kimarekani bilioni 185.2 katika kipindi cha Januari hadi Septemba, na kufikia kiwango cha juu zaidi katika historia kwa kipindi kama hicho.

Qian Keming, Naibu Waziri wa Biashara wa China, alisema kuwa tangu Mwaka 2000, China imeagiza bidhaa zenye thamani ya dola za kimarekani trilioni 1.2 kutoka Afrika na kusafirisha bidhaa zenye thamani ya dola za kimarekani trilioni 1.27 barani Afrika. Aliongeza kuwa China imekuwa ikijitahidi kuongeza uagizaji bidhaa kutoka Afrika.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha