Rais Xi atangaza kuipatia Afrika dozi bilioni 1 za chanjo dhidi ya UVIKO-19, na kuahidi utekelezaji wa miradi tisa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 30, 2021
Rais Xi atangaza kuipatia Afrika dozi bilioni 1 za chanjo dhidi ya UVIKO-19, na kuahidi utekelezaji wa miradi tisa
Rais Xi Jinping wa China akitoa hotuba kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) kwa njia ya video, hapa Bejing, Mji Mkuu wa China Novemba 29, 2021 (Xinhua/Huang Jingwen)

BEIJING - Rais wa China Xi Jinping ametangaza kwamba China itatoa dozi zaidi ya bilioni 1 za chanjo dhidi ya UVIKO-19 kwa Afrika na kuahidi kutekeleza kwa pamoja miradi tisa ya ushirikiano wa siku zijazo kati ya China na Afrika.

"Nina hakika kwamba juhudi za pamoja za China na Afrika zitafanikisha Mkutano huu wa FOCAC, utakaounganisha nguvu kuu za Wachina na Waafrika bilioni 2.7 na kutuongoza kuelekea jumuiya ya ngazi ya juu yenye mustakabali wa pamoja wa siku zijazo kati ya China na Afrika," Xi amesema Jumatatu ya wiki hii wakati akihutubia ufunguzi wa Mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) kwa njia ya video.

MSHIKAMANO WA KUPAMBANA NA JANGA LA UVIKO-19

Ili kusaidia Umoja wa Afrika (AU) kutimiza lengo lake la kuchanja chanjo dhidi ya UVIKO-19 asilimia 60 ya watu wa Afrika ifikapo Mwaka 2022, Rais Xi ametangaza kuwa China itatoa dozi nyingine bilioni moja za chanjo kwa Afrika, kati ya hizo, dozi milioni 600 zitatolewa kama msaada na dozi milioni 400 zitatolewa kupitia uzalishaji wa pamoja wa kampuni za China na nchi husika za Afrika.

"Pamoja na hayo, China itatekeleza miradi 10 ya matibabu na afya kwa nchi za Afrika, na kutuma wataalamu wa afya ya umma na madaktari 1,500 barani Afrika," Xi ameongeza.

Hadi kufikia Novemba 12, 2021, China ilikuwa imetoa zaidi ya dozi bilioni 1.7 za chanjo dhidi ya UVIKO-19 kwa zaidi ya nchi na mashirika 110, zikiwemo nchi 50 za Afrika na Tume ya AU.

MATARAJIO MAPYA

"Tunahitaji kufungua matarajio mapya ya ushirikiano kati ya China na Afrika, kupanua biashara na uwekezaji, kubadilishana uzoefu katika kupunguza umaskini, kuimarisha ushirikiano katika uchumi wa kidijitali, kukuza ujasiriamali kwa vijana wa Afrika na maendeleo ya biashara ndogo na za kati (SMEs)” Xi amebainisha huku akitoa wito wa kuimarisha ushirikiano wa kivitendo kati ya pande hizo mbili.

Xi amebainisha kwamba, China itatekeleza miradi 10 ya kupunguza umaskini na kilimo barani Afrika, kutoa dola za kimarekani bilioni 10 za kuwezesha biashara ili kusaidia mauzo ya nje ya Afrika, na kujenga Eneo la kielelezo la ushirikiano wa kina wa kibiashara na kiuchumi kati ya China na Afrika na Eneo la viwanda la ushirikiano wa Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia moja” kati ya Afrika na China nchini China.

Amesisitiza kwamba, China itahimiza kampuni zake kuwekeza dola za kimarekani zisizopungua bilioni 10 barani Afrika katika miaka mitatu ijayo, kutekeleza miradi 10 ya uchumi wa kidijitali barani Afrika, kutekeleza miradi 10 ya maendeleo yasiyochafua mazingira, ulinzi wa mazingira na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa Afrika, kusaidia kujenga au kukarabati shule 10 barani Afrika, na kuwaalika wataalamu 10,000 wa ngazi ya juu wa Afrika kwenye semina na warsha.

JUMUIYA YENYE MUSTAKABALI WA PAMOJA KATIKA ENZI MPYA

Wakati wa ufunguzi wa mkutano huo wa nane wa mawaziri wa FOCAC, Xi ametoa mapendekezo manne ya kujenga jumuiya yenye mustakabali wa pamoja kati ya China na Afrika katika enzi mpya, akitoa wito kwa pande zote mbili kupambana na UVIKO-19 kwa mshikamano, kuimarisha ushirikiano wa kivitendo, kukuza maendeleo yasiyo na uchafuzi kwa mazingira, na kudumisha usawa na haki.

Kwa upande wake Rais wa Senegal, nchi mwenyeji wa Mkutano huo wa FOCAC kwa Mwaka 2021 amesema, tangu kuanzishwa kwa FOCAC miaka 21 iliyopita, China na watu wake wameshirikiana na nchi za Afrika pamoja na watu wake kwa kuzingatia kanuni za urafiki, mshikamano, kuaminiana na kuheshimiana.

Mkutano huo wa siku mbili uliopangwa kufanyika Novemba 29-30 katika Mji Mkuu wa Senegal Dakar, unatarajiwa kutathmini utekelezaji wa matokeo ya Mkutano wa Beijing wa FOCAC wa Mwaka 2018 na kufungua matarajio mapya ya ushirikiano kati ya China na Afrika.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha