Rais wa Jamhuri ya Kongo akutana na Mwanadiplomasia wa juu wa China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 06, 2021

Rais wa Jamhuri ya Kongo Denis Sassou Nguesso (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Yang Jiechi, Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Mkurugenzi wa Ofisi ya Kamati ya Mambo ya Nje ya Kamati Kuu ya CPC, huko Brazzaville, Jamhuri ya Kongo, Desemba 5, 2021. (Xinhua/Shi Yu)

BRAZZAVILLE - Rais wa Jamhuri ya Kongo Denis Sassou Nguesso amekutana na kufanya mazungumzo na Yang Jiechi, Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Mkurugenzi wa Ofisi ya Mambo ya Nje ya Kamati Kuu ya CPC.

Katika mkutano wao wa Jumapili ya wiki iliyopita, Yang amewasilisha salamu za Rais Xi Jinping wa China kwa Rais Sassou. Na kusema kwamba, kwa uangalizi na uongozi wa wakuu wa nchi hizo mbili, uhusiano na ushirikiano wa kimkakati wa pande zote kati ya nchi hizo mbili umepata maendeleo makubwa.

Yang amebainisha kwamba, China inapenda kuimarisha mawasiliano ya hali ya juu na Jamhuri ya Kongo, na kuungana mkono kithabiti katika masuala makuu ya msingi, ili kuonesha umaalumu na kiwango cha juu cha uhusiano na ushirikiano wa kimkakati wa pande zote kati ya nchi hizo.

Ameongeza kuwa, China itatumia fursa ya utekelezaji wa matokeo ya Mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) kuendelea kuiunga mkono Jamhuri ya Kongo katika mapambano dhidi ya janga la UVIKO-19, kutafuta na kukuza zaidi ushirikiano mpya kwa utaratibu katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na miundombinu na maeneo ya uwekezaji wa viwanda, ili kutoa mchango kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Jamhuri ya Kongo.

Kwa upande wake, Rais Sassou alimwomba Yang kuwasilisha salamu zake za heri kwa Rais Xi Jinping, na kumpongeza kwa maadhimisho ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa CPC. Amesema kwamba, Jamhuri ya Kongo inathamini sana uhusiano na ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili na kuishukuru China kwa kutoa msaada muhimu kwa mapambano dhidi ya UVIKO-19 na kufufua uchumi.

Sassou amesema, Jamhuri ya Kongo inafuata sera ya kuwepo kwa China moja na inapenda kukuza hali ya kuaminiana ya kisiasa kati yake na China, na kuongeza kuwa nchi yake inatarajia kutafuta ushirikiano na China katika nyanja tofauti, zikiwemo nishati, usindikaji, usafiri, na kilimo.

Katika ziara yake hiyo nchini Jamhuri ya Kongo, Yang pia alikutana na Jean-Claude Gakosso, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kongo siku ya Jumapili ya wiki iliyopita.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha