

Lugha Nyingine
Adama Barrow achaguliwa tena kuwa Rais wa Gambia
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi (IEC) ya Gambia, Alieu Momar Njie, Jumapili ya wiki iliyopita alitangaza kuwa Adama Barrow, Kiongozi wa Chama cha Taifa cha Wananchi (NPP) ameshinda kwenye uchaguzi wa Rais uliofanyika Jumamosi ya wiki iliyoisha.
Desemba 4, Gambia ilifanya uchaguzi wa Rais, ambapo wagombea sita akiwemo Rais wa sasa Adama Barrow waliwania kiti cha nafasi ya urais wa awamu ijayo.
Barrow alipata jumla ya kura halali 457,519 ambayo ilichukua asilimia 53 ya jumla ya kura zote zilizopigwa. Alimshinda mshindani wake mkuu Ousainu Darboe wa Chama cha United Democratic Party (UDP) ambaye alipata kura 238,253.
Barrow alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Rais wa Gambia mnamo Mwaka 2016 huku akiongoza muungano wa vyama saba vya kisiasa na baadhi ya wagombea huru, na alimshinda mtangulizi wake Yahya Jammeh.
Kabla ya kuchaguliwa kwake tena, Barro aliahidi kuboresha maendeleo ya kilimo na ya miundombinu ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa takwimu za Tume Huru ya Uchaguzi ya Taifa la Gambia, wapiga kura zaidi ya laki 9 walijiandikisha kushiriki kwenye uchaguzi huo. Zoezi la kupiga kura lilianza saa mbili ya Tarehe 4 ya saa za huko na kuisha saa kumi na moja ambapo wapiga kura walipiga kura katika vituo 1554.
Jamhuri ya Gambia iko Magharibi mwa Afrika, na ina idadi ya watu wapatao milioni 2.2.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma