Nchi mbalimbali za Afrika zalaani marufuku ya usafiri kutokana na kirusi cha Omicron

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 07, 2021

ABUJA – Serikali ya Nigeria imekosoa uamuzi wa Serikali ya Uingereza wa kupiga marufuku abiria kutoka Nigeria kutokana na kugunduliwa kwa visa vya maambukizi ya virusi vya korona aina ya Omicron katika nchi hiyo yenye watu wengi zaidi barani Afrika.

Lai Mohammed, Waziri wa Habari na Utamaduni wa Nigeria aliwaambia waandishi wa habari Jumatatu ya wiki hii kwamba, uamuzi wa Serikali ya Uingereza wa kuiweka Nigeria kwenye orodha ‘nyekundu’ ya nchi ambazo wasafiri wake hawaruhusiwi kuingia nchini Uingereza hausukumwi na sayansi na lazima ufutwe mara moja hasa ikizingatiwa kirusi cha korona aina ya Omicron hakijaanzia Nigeria.

"Unashutumuje aina hii ya hatua inayobagua nchi yenye watu milioni 200, kwa sababu tu ya visa vichache vya COVID-19?" Mohammed aliwaambia waandishi wa habari, huku akiuelezea uamuzi wa Serikali ya Uingereza kama "usiyo wa haki, usio wa usawa, wa kuadhibu, na usiyoweza kutetewa".

Serikali ya Uingereza ilitangaza mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa itasitisha kufanya maamuzi juu ya maombi ya visa ya wageni kutoka nchi zote za orodha nyekundu, ikiwa ni pamoja na Nigeria. Pia walizuia abiria wanaoingia kutoka Nigeria, kuanzia Jumatatu ya wiki hii.

Nchi mbalimbali za Magharibi zimechukua hatua kama hizo za Uingereza, hali ambayo imeamsha hisia kali miongoni mwa viongozi wa Afrika.

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini wakati akihutubia kwenye mkutano uliofanyika mjini Dakar, Senegal Jumatatu ya wiki hii ametupa lawama kwa nchi za Magharibi kwa kile alichodai nchi hizo zinaadhibu nchi za Afrika kwa kutanguliza sayansi katika kupambana dhidi ya Janga la UVIKO-19.

"Jambo lingine la kukatisha tamaa lililotupata, wakati wanasayansi wa Afrika Kusini walipogundua kirusi cha Korona aina ya Omicron, mara moja walichukua jukumu la kufahamisha ulimwengu mzima kwamba kuna aina mpya ya kirusi" Ramaphosa amesema, na kuongeza: “Na jibu lilikuwa nini? Nchi za Magharibi ziliamua kuadhibu Afrika kwa kuweka marufuku ya usafiri”.

"Unajiuliza, sayansi iko wapi. Siku zote walituambia, msingi wa maamuzi uko katika sayansi, lakini wakati linapokuja suala la wao kuwa kisayansi zaidi hawafanyi hivyo" Ramaphosa amesema.

Naye Rais wa Senegal Mackay Sall, katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo, alionya kwamba nchi za Magharibi zinahatarisha nchi kuficha habari juu ya UVIKO-19 kwa kuhofia athari zinazoweza kutokea. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha