

Lugha Nyingine
China inaweza kufikia malengo makuu ya kiuchumi ya mwaka: Waziri Mkuu Li (3)
![]() |
Waziri Mkuu wa China Li Keqiang akiwa katika mkutano wa mtandaoni na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia David Malpass mjini Beijing, Mji Mkuu wa China, Desemba 13, 2021. (Xinhua/Yin Bogu) |
BEIJING - Waziri Mkuu wa China Li Keqiang amesema kuwa China inaweza kufikia malengo makuu ya mwaka ya kiuchumi na kwamba nchi hiyo iko tayari kushirikiana na Benki ya Dunia ili kuimarisha ushirikiano katika mitaji na ujuzi ili kusaidia ushirikiano wa pande nyingi na malengo ya maendeleo ya kimataifa.
Li ameyasema hayo Jumatatu ya wiki hii katika mkutano wa mtandaoni na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia, David Malpass, mjini Beijing.
Akizungumzia Mkutano Mkuu wa mwaka wa Kazi ya Uchumi wa China uliomalizika hivi karibuni, Li amesema kama nchi kubwa zaidi inayoendelea duniani, kazi ya uchumi ya China mwaka ujao ni kuweka kipaumbele kwa utulivu wakati wa kutafuta maendeleo.
Amebainisha kwamba, kutokana na China kukabiliwa na shinikizo la kushuka kwa uchumi, itatoa kipaumbele katika kuratibu ukuaji madhubuti wa uchumi, sambamba na kurekebisha muundo wa uchumi na kukuza mageuzi ya uchumi.
Li amesema kwamba China itaimarisha uaminifu kwa uchumi wake, pia itakabiliana na changamoto. Akitoa maelezo kuhusu sera ya uchumi ya China, Li amesisitiza kwamba hatua zitakazochukuliwa na Serikali zitalinda uthabiti wa sera ya jumla ya uchumi na kutekeleza kwa ufanisi sera za kifedha.
Ameeleza kwamba, sera imara za kifedha zinapaswa kuwa na unyumbufu, na kudumisha ukwasi katika kiwango mwafaka.
Amesisitiza kwamba, China itaongeza huduma za kifedha zinazojumuisha mashirika ya soko, hasa kampuni ndogo, za kati na ujasiriamali, na kuongeza uthabiti na imani ya uchumi wa China.
Huku akibainisha kuwa Benki ya Dunia ni shirika muhimu la pande nyingi katika mambo ya maendeleo ya kimataifa, Li amesema uhusiano kati ya China na Benki ya Dunia hudumisha maendeleo mazuri. Na kwamba, China inaunga mkono mazungumzo ya awamu ya 20 ya kuongeza fedha kwa ajili ya Muungano wa Maendeleo ya Kimataifa (IDA).
Kwa upande wake, Malpass amesifu maendeleo tulivu ya kiuchumi ya China na akapongeza uhusiano mzuri kati ya Benki ya Dunia na China.
Malpass amesema Benki ya Dunia iko tayari kufanya ushirikiano na China katika mikopo, kupunguza umaskini, na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Malpass ametoa shukrani zake kwa msaada wa China katika mazungumzo ya kuongeza fedha kwenye IDA.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma