

Lugha Nyingine
Kampuni ya Wachina yawapa wafanyabiashara wadogo wa bidhaa za chakula wa Zambia maeneo safi na salama ya biashara (2)
![]() |
Maria Mukela, mfanyabiashara wa mazao ya chakula, akionesha nafaka katika Soko la Mazao ya Chakula la JCS huko Lusaka, Zambia, Desemba 18, 2021. Upatikanaji wa maeneo ya biashara yenye hadhi ni changamoto kwa wafanyabiashara wengi wadogo wa mazao ya chakula nchini Zambia. Ni kwa sababu hii Kampuni ya Jihai Central Sports (JCS), inayomilikiwa na Wachina inayofanya biashara nchini Zambia, iliamua kuwawezesha wafanyabiashara wadogo wa mazao ya chakula mjini Lusaka kwa kuwapa maeneo safi na ya bei nafuu ya biashara. (Picha na Lillian Banda/Xinhua) |
LUSAKA - Upatikanaji wa maeneo ya biashara yaliyo safi ni changamoto kwa wafanyabiashara wengi wadogo wa bidhaa za chakula nchini Zambia.
Ni kwa sababu hii Kampuni ya Jihai Central Sports (JCS), inayomilikiwa na Wachina ambayo inafanya biashara nchini Zambia, iliamua kuwawezesha wafanyabiashara wadogo wa bidhaa za chakula huko Lusaka, Mji Mkuu wa Zambia kwa kuwapa maeneo safi na ya bei nafuu ya kufanya biashara.
Soko la Chakula la JCS ni mpango wa JCS, eneo la biashara ambalo linapatikana katika eneo la Longacres la Lusaka.
Mmoja wa wafanyabiashara hao Maria Mukela mwenye umri wa miaka 48 ambaye amejikita katika uuzaji wa aina mbalimbali za bidhaa za nafaka alieleza kuwa kituo hicho cha biashara ni cha kipekee kwa kuwapa wafanyabiashara mazingira mazuri ya kufanyia kazi ambayo yanakuza biashara zao.
"Sehemu hii ni safi na wafanyabiashara wanapata maeneo safi ya kufanyia biashara pamoja na vifaa vya usafi wa mazingira. Ndiyo maana soko hili la bidhaa za chakula linavutia wateja busara na wenye hadhi" anasema Mukela, ambaye amekuwa akifanya biashara katika Soko la bidhaa za Chakula la JCS kwa takriban miaka sita.
Ameongeza kuwa Soko la bidhaa za Chakula la JCS pia hutumika kama jukwaa la kutoa fursa kubwa za kibiashara kwa wafanyabiashara wadogo wa bidhaa za chakula.
"Nimepewa kandarasi za kusambaza kiasi kikubwa cha vyakula vya nafaka kwa mashirika ya kibinafsi na ya umma. Hii imeniwezesha kukuza biashara yangu," Mukela amebainisha.
Kwa upande wake, Doreen Soniso mwenye umri wa miaka 36 ambaye amekuwa akifanya biashara katika Soko la JCS kwa takriban miaka mitano sasa, anasema nafasi hiyo imempa fursa ya kufanya biashara katika mazingira safi na salama.
"Sina wasiwasi wa kuhama kutoka sehemu moja hadi nyingine hasa wakati wa mvua kama ilivyo kwa wafanyabiashara wadogo wanaojishughulisha na biashara ya bidhaa za chakula na wanaoendesha shughuli zao mitaani," Songisio ameeleza.
Anaongeza kuwa Soko la bidhaa za Chakula la JCS linawapa wafanyabiashara wadogo fursa ya kuwasiliana na watu wa nchi mbalimbali na wenye hali tofauti, jambo ambalo ni muhimu kwa wafanyabiashara wanaotaka kujihusisha na biashara ya kimataifa.
Kwa mujibu wa Meneja wa Soko la bidhaa za Chakula la JCS Billy Ng'ambi, kuna takriban wafanyabiashara wadogo 39, wengi wao wakiwa ni Wazambia ambao wamepewa maeneo ya kufanyia biashara katika kituo hicho.
"Tuna wafanyabiashara 26 wanaofanya biashara ya matunda na mboga mboga na 13 wanafanya biashara za aina mbalimbali za vyakula vya nafaka. Mazao hayo yanatoka ndani na nje ya nchi," Ng'ambi amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma